Historia ya Tume
Tume ya Utumishi wa Walimu imepitia hatua mbalimbali katika uanzishwaji wake. Hatua hizo ni kama zifuatazo :-
IDARA YA UTUMISHI WA WALIMU
Kufuatia Sera ya Ajira na Menejimenti katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1999, Utumishi wa Umma uliunganishwa. Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002 ilianzishwa na kufuta iliyokuwa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Namba 1 ya mwaka 1989. Tume ilifanywa kuwa Idara ya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) chini ya Kifungu cha Sheria 15(1), (b). Idara ilishughulikia majukumu yote yaliyokuwa yakitekelezwa na TSC kwa walimu walioajiriwa katika Shule za Serikali.
Hata hivyo, kwa Marekebisho ya Sheria Namba 18 ya mwaka 2007, Tume ya Utumishi wa Umma ilifanywa kuwa rekebu, na Idara ya Utumishi wa Walimu iliendelea kuwa tendaji. Mfumo huo ulileta changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya TSD chini ya Chombo cha Urekebu. Aidha, changamoto kubwa iliyoikabili TSD ilikuwa ni upungufu mkubwa wa rasilimali fedha na watu. Pia, kulikuwa na changamoto ya rufaa za walimu dhidi ya uamuzi wa Idara kushughulikiwa na Tume ya Utumishi wa Umma. Serikali iliona utumishi wa walimu upewe umuhimu wa kipekee kutokana na wingi wao, upekee wa majukumu na changamoto nyingine zilizokwishajitokeza.
TUME YA UTUMISHI WA WALIMU
Taarifa ya Tume ya Rais ya Elimu chini ya Mheshimiwa Jackson Makweta (1980-82) ilibaini kwamba, suala la usimamizi wa utumishi wa walimu lilikuwa na changamoto. Kadri Walimu walivyokuwa wakiongezeka, matatizo ya kukosa huduma ipasavyo yalikuwa yakiongezeka pia. Tume hiyo iliiona changamoto ya UTS kuwa kitengo kidogo kwenye iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni na Ofisi za Wakurugenzi wa Maendeleo wa Mikoa na Wilaya. Waliona kuwa, Muundo huo usingeweza kukabiliana na ongezeko kubwa la walimu na changamoto zilizokuwa zimebainishwa.
Sheria Na. 1 ya Mwaka 1989 ilianzisha Tume ya Utumishi wa Walimu (Teachers’ Service Commission) ambayo ilikuwa ni Idara inayojitegemea chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni. Majukumu yote yaliyokuwa yakitekelezwa na UTS yalihamishiwa TSC.
HUDUMA KWA WALIMU
Serikali iliamua kuunganisha utumishi wa walimu wote wa Serikali na wa Sekta binafsi chini ya Sheria Na. 6 ya mwaka 1962 ya Huduma kwa Walimu (Unified Teaching Service – UTS).
UTS ilishughulikia utumishi wa walimu wote wa Serikali na Waajiri wengine katika masuala yaliyohusu Ajira, kuthibitishwa kazini, kupandishwa cheo na Maadili na Nidhamu. Mwalimu aliyeajiriwa na Mwajiri mwingine nje ya Serikali, alijaza mkataba na Mwajiri wake na kuuwasilisha UTS kwa ajili ya kusajiliwa na kupewa namba ya usajili (UTS No.). Mapendekezo ya kuthibitishwa kazini na kupandishwa cheo yaliwasilishwa UTS, na Waajiri wote walitekeleza uamuzi uliotolewa na UTS.
Nguzo za Maadili ya Kazi ya Ualimu ziliandaliwa na kufundishwa kwenye Vyuo vya Ualimu. Aidha, kila Mwalimu alipaswa kuzingatia nguzo hizo bila kujali aina ya Mwajiri. Mwalimu yeyote aliyevunja Maadili ya Kazi ya Ualimu au kuwa na utovu wowote wa nidhamu aliadhibiwa chini ya masharti ya UTS.
TUME YA UTUMISHI WA WALIMU
Sheria Namba 25 ya Mwaka 2015 ilianzisha Tume ya Utumishi wa Walimu. Walimu wanaoshughulikiwa chini ya Sheria hii ni Walimu waajiriwa wa Serikali wanaofundisha katika Shule za Msingi na Sekondari kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Majukumu ya Tume yametajwa kwenye kifungu cha 5 cha Sheria.
Suala la Maadili na Nidhamu kwa Walimu limeendelea kuwa chini ya Tume ya Utumishi wa Walimu, ikiwa ni kufafanua na kusimamia Maadili, Miiko na Nidhamu ya kazi ya Ualimu.