ZINGATIENI TARATIBU KATIKA KUSHUGHULIKIA MASHAURI YA NIDHAMU YA WALIMU: KATIBU TSC
Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Sura 448, Ofisi za TSC ngazi ya Wilaya ni Mamlaka ya kushughulikia mashauri ya nidhamu ya walimu pamoja na rufaa za walimu zinazotokana na uamuzi unaofanywa na mamlaka ya kwanza ya nidhamu ambayo ni Wakuu wa Shule.
Uamuzi wa mashauri pamoja na rufaa za walimu unaofikiwa na Kamati za TSC Wilaya unafanyika baada ya hatua mbalimbali zilizowekwa kuzingatiwa, na ili uamuzi uwe wa haki ni lazima hatua zote za shauri zifuate sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka makosa yanaweza kuharibu shauri.
Katika kuazimisha mwaka mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alifanya ziara katika ofisi mbalimbali za TSC Wilaya ambapo moja ya mabo aliyoyasisitiza kwa watumishi wa TSC ni kuhakikisha wanazingatia taratibu zote katika kushughulikia mashauri ya walimu.
Akiwa wilayani Songwe, Nkwama alisema kuwa katika rufaa zinazokatwa Tume makao Makuu baada ya warufani kutoridhishwa na uamuzi wa TSC ngazi ya Wilaya moja ya mabo yaliyobainika ni kutozingatiwa kwa taratibu kitu ninachosababisha kutotendeka kwa haki.
Alifafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kushughulikia masuala ya walimu kwa haki na weledi hivyo ni wajibu wa watumishi wa tume hiyo kuzisoma na kuzielewa sheria na kanuni ili waweze kuzishauri vyema kamati za Wilaya wakati wa kufanya maamuzi ya mashauri ya walimu.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametuweka ili tumsaidie katika kutekeleza majukumu yanayohusu utumishi wa walimu. Ukiangalia katika kipindi hiki cha mwaka mmoja Rais amefanya mambo mengi ya kuwaletea maendeleo wananchi, hivyo nasisi moja ya maendeleo tunayopaswa kuyafanya katika kuboresha utumishi wa walimu ni kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili tutende haki wakati wote,” alisema Nkwama.
“Katika rufaa tunazopokea, tumeona kwamba kuna kutokuzingatiwa kwa sheria na kanuni katika kushughulikia mashauri haya. Na kule Makao Makuu Tume inapitia kila kipengele kwa umakini ili kuona kama kila hatua ilizingatia sheria. Matokeo yake tumekuta warufani wanashinda kutokana na udhaifu katika kuzingatia taratibu uliofanyika huku wilayani. Kosa linaweza kuwepo, lakini ukikosea kuzingatia taratibu kesi yote inaharibika,” alisema.
Kiongozi huyo aliendelea kueleza kuwa miongoni mwa taratibu za kuzingatia ni uandishi wa hati ya mashtaka ambayo inatakiwa kuelezea kwa ufasaha wakati, mahali na namna kosa lilivyotendwa huku ikionesha kosa hilo limekiuka kifungu gani cha sheria/kanuni.
Aidha, endapo shauri limeundiwa kamati ya uchunguzi ni lazima mtuhumiwa apewe wito wa kuhudhuria kwenye kikao cha kamati hiyo, ni lazima uwepo ushahidi kuwa mtuhumiwa amepokea barua ya wito na wakati wa kikao mtuhumiwa apewe nafasi ya kuwahoji mashahidi na kuona nyaraka zote zinazotumia kama ushahidi dhidi yake.
“Kuna changamoto kwenye kuitwa kwa mtuhumiwa kwenye kamati ya uchunguzi, mara nyingi tunaona barua ya wito imeandikwa lakini hatuoni ushahidi wa mtuhumiwa kupokea wito huo. Wengi wanaandika barua ya kumwita mtuhumiwa lakini hawachukui hatu za ziada kuhakikisha barua ya wito inamfikia mhusika,” alisema.
Vilevile, aliwataka watumishi hao kuhakikisha wanatunza nyaraka za ofisi vizuri kwa ajili ya kumbukumbu na pale zinapohitajika kwa ajili ya matumizi mengine ziweze kupatikana kwa urahisi ili kusaidia shughuli zingine zinazotegemea nyaraka hizo ziweze kufanyika.
“Wote mnajua kwamba mwalimu anapokata rufaa Tume Makao Makuu, kitu cha kwanza tunachofanya ni kuwataka muwasilishe nyaraka zote za shauri hilo, maana hatuwezi kushughulikia rufaa bila kupata nyaraka za shauri kutoka wilayani. Sasa inashangaza unapoagiza nyaraka inachukua miezi nyaraka haziletwi, hii siyo sawa hata kidogo, ni lazima tubadilike,” alisema.
Naye Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Songwe, Issa Shemgei Shehagilo alisema Wilaya ya Songwe ina jumla ya shule za msingi 56 na za sekondari 11 za Serikali huku ikiwa na jumla ya walimu wa shule za msingi 458 na shule za sekondari 175 wanaohudumiwa na TSC kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448.
Akielezea mafanikio ya TSC Wilaya ya Songwe katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, Shehagilo alisema kuwa mwaka 2020/2021 jumla ya walimu 245 walipandishwa vyeo ambapo katika idadi hiyo walimu 153 ni wa shule za msingi na 92 ni wa sekondari huku walimu 25 wakibadilishiwa kazi/cheo baada ya kujiendeleza kimasomo.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu kutokana na maelekezo yake hakuna mwalimu aliyestahili kupandishwa ambaye alisahaulika. Walimu wote 245 tuliowapandisha walibadilishiwa mishahara na kuanza kupokea mishahara ya vyeo vipya ndani ya muda mfupi tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma,” alisema Shehagilo.
Kwa upande wa nidhamu kwa walimu, Shehagilo alisema kuwa nidhamu ya walimu imeendelea kuwa nzuri kwani kwa mwaka 2020/2021 ofisi hiyo ilikuwa na shauri moja tu na kwa mwaka 2021/2022 kuna mashauri matatu huku akieleza kuwa mafanikio hayo ni kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuiwezesha TSC kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuwafikia walimu na kuwapatia elimu kuhusu utumishi wao.
“Tumefanikiwa kusambaza vijitabu vya Kanuni za Maadili ya Kazi ya Ualimu kwa shule 56 za msingi na 11 za sekondari. Tumefanya ziara kwenye shule 23, pia tumeendelea kufanya semina na mikutano kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakuu wa shule kuhusu majukumu yao wakiwa ni mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa walimu. Vilevie, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwani kupitia uongozi wake tumefanikiwa kuwafikia walimu 458 na kuwapa elimu juu ya masuala ya utumishi wao,” alisema.
Katika ziara hiyo, watumishi wa TSC Songwe walipata fursa ya kukumbushwa masuala mbalimbali ya kiutumishi yakiwemo namna ya kuandika barua za Serikali kwa kuzingatia Miongozo iliyopo, namna ya kutunza nyaraka za ofisi pamoja namna bora ya kushughulikia masuala ya Ajira, Maendeleo na Nidhamu ya walimu.