MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN UMEKUWA WA NEEMA KWA WALIMU BUTIAMA

20 Apr, 2022
MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN UMEKUWA WA NEEMA KWA WALIMU BUTIAMA

Wakati mafanikio ya utendaji wa kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yakionekana katika sekta mbalimbali ikiwa ni mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Ofisi ya TSC Wilaya ya Butiama imekiri kuimarika kwa nidhamu, kuongezeka kwa morali ya kazi na kupungua kwa malalamiko kwa walimu wa wilaya hiyo.

Mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha utumishi wa walimu huku lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha walimu wanakuwa na mazingira bora ya kazi ili waweze kutoa huduma bora ya kufundisha wanafunzi.

Regina Donatus Kinabo ni Afisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) anayeshughulikia masuala ya Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu katika Wilaya ya Butiama ambaye alifanya mahojiano na Jarida hili kwa niaba ya Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wa wilaya hiyo ambapo alibainisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kutokana na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Kinabo alianza kwa kueleza kuwa, walimu wote waliokuwa na sifa za kupanda vyeo/madaraji katika wilaya hiyo walipandishwa kwa asilimia 100 kitu ambacho hakikuwahi kutokea katia utumishi wa walimu katika miaka ya hivi karibuni.

“Hatujawahi kushuhudia upandishaji wa madaraja ukifanyika kwa mafanikio kama ule wa mwezi Juni 2021. Huko nyuma tulikuwa na changamoto sana kwenye eneo hili, kwa mfano katika zoezi la upandishaji madaraja la mwaka 2019 walimu waliokuwa na sifa za kupandishwa walikuwa 399 lakini ikama ilikuwa na nafasi 57 tu, hivyo walimu 342 hawakupandishwa pamoja na kwamba walikuwa na sifa,” alisema Kinabo.

Afisa huyo alifafanua kuwa katika zoezi la upandishaji vyeo lililofanyika katika mwaka wa fedha 2020/2021 chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, TSC Butiama ilipandisha walimu 641 wa Shule za Msingi na walimu 265 wa Shule za Sekondari na kufanya jumla ya walimu waliopanda madaraja kwa mwaka huo kuwa 906 ambapo idadi hiyo ilihusisha walimu 399 ambao hawakupandishwa mwaka 2019.

Tofauti na siku za nyuma, Ofisi ya TSC Wilaya ya Butiama ilifanikiwa kuwabadilishia kazi/cheo walimu 151 ambao ndio waliowasilisha maombi ya kubadilishiwa kazi/cheo baada ya kujiendeleza kimasomo na kukidhi vigezo vingine vya kufanyiwa mabadiliko hayo kwa mujibu wa Sheria Kanuni na Taratibu za Tume ya Utumishi wa Walimu.

“Tunamshukuru Rais wetu kwa kuendelea kuwajali walimu kwani baada ya zoezi la upandishaji wa madaraja kukamilika aliruhusu walimu wenye sifa kubadilishiwa kazi/cheo. Hii ilisaidia sana kuleta utulivu kwa walimu wetu kwani kulikuwa na wimbi kubwa la walimu waliokuwa wanahitaji kufanyiwa mabadiliko hayo kwa muda mrefu bila mafanikio,” alisema Kinabo.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ofisi hiyo imeendelea kushughulikia vibali vya kustaafu kazi ya ualimu ambapo imetoa vibali kwa walimu 15, katika idadi hiyo walimu 3 wanastaafu kwa hiari na walimu 12 wanastaafu kwa lazima baadi ya kufikia ukomo wa utumishi wao kwa mujibu wa sheria.

“Tumeendelea kuwashughulikia walimu wanaostaafu kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa nyaraka zao zipo vizuri na kuwapatia vibali kwa wakati ili kuwaepushia usumbufu katika kushughulikia mafao yao. Tunashukuru kwani tumeendelea kutekeleza jukumu hili kwa weledi na hata walimu wanapowasilisha nyaraka zao kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wamekuwa wakipata mafao yao ndani ya muda mfupi tofauti na zamani,” alisema.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani ofisi hiyo imefanikiwa kuendelea kuwafikia walimu katika maeneo yao na kutoa elimu juu ya masuala ya mbalimbali ya utumishi wao kitu ambacho kimesaidia kuimrika kwa nidhamu na kupungua kwa mashauri ya nidhamu ya walimu.

“Tumefanikiwa kutembelea shule 31 za Msingi na Sekondari, tumefanya kikao na Wakuu wa Shule 88 na Shule Shikizi 5 pamoja na Maafisa Elimu Kata 18. Tumezungumzia masuala ya Maadili ya Kazi ya Ualimu na kuhakikisha kila mwalimu anapata nakala ya kijitabu cha masuala hayo. Pia tumewakumbusha Wakuu wa Shule wajibu wao wakiwa ni mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa walimu pamoja na namna ya kuandaa hati ya mashtaka na notisi. Vilevile, tumewafunsisha walimu taratibu na namna ya kukata rufaa pale inapotokea hawajaridhika na uamuzi ya shauri la nidhamu,” alisema.

Alihitimisha kwa kueleza kuwa mashauri ya nidhamu yamepungua kutoka 23 mwaka 2017/2018 hadi shauri 1 mwaka 2021/2022 na hivyo kufanya walimu kuongeza kasi ya uwajibikaji na kuifanya Wilaya hiyo kuendelea kuongeza kiwango cha ufaulu katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kufanikiwa kupata Tuzo za Ubora wa Taaluma kwa matokeo ya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita zilizotolewa hivi karibuni.