WATUMISHI TSC WATAKIWA KUACHA MIGOGORO NA MIVUTANO KAZINI INAYOKWAMISHA MALENGO YA SERIKALI YA KUTOA HUDUMA BORA KWA WALIMU

08 Apr, 2022
WATUMISHI TSC WATAKIWA KUACHA MIGOGORO NA MIVUTANO KAZINI INAYOKWAMISHA MALENGO YA SERIKALI YA KUTOA HUDUMA BORA KWA WALIMU

Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuachana na migogoro na mivutano ambayo inakwamisha utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo na kusababisha kutofikiwa kwa malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha utumishi wa walimu.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Katibu wa TSC, Paulina Nkwama wakati alipotembelea ofisi za TSC Wilaya ya Momba iliyopo mkoani Songwe kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya TSC katika wilaya hiyo ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.

Nkwama alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina matarajio kuwa TSC itakuwa suluhisho la changamoto za walimu, hivyo ni lazima kila mtumishi wa tume hiyo afanye kazi kwa bidii, nidhamu, weledi na mshikamo kuku akisisitiza kuwa kamwe hatamvumilia mtumishi atakayekuwa chanzo cha migogoro na mivutano kazini.

“Tumewekwa na Rais ili tuwahudumie wananchi na sisi TSC wananchi wetu ni walimu. Tuna jukumu kubwa sana kwani mwalimu anapoingia kwenye ajira hadi anapohitimisha utumishi wake yupo mikononi mwetu. Sisi tunaweza kumfanya aipende kazi yake au aichukie, awe na nidhamu au mtovu wa nidhamu, atengeneze Taifa bora la kesho au Taifa bovu.”

“Hivyo, ili kuweza kuyafanya hayo yote kwa ufanisi ni lazima tuweze kuwajibika ipasavyo. Zipo baadhi ya ofisi zetu ambazo wao kila kukicha ni migogoro isiyokwisha. Kama ndani ya ofisi hamuelewani ni lazima wateja (walimu) wataathirika, na mimi sipo tayari kuona mwalimu yoyote anapata shida kwa sabau ya watendaji wa ofisi yangu,” Nkwama alisema.

Aliendelea kueleza kuwa Ofisi za Wilaya ndiyo moyo wa TSC kwani kwa mujibu wa sheria ndizo zenye mamlaka ya kushughulikia masuala ya Ajira na Maendeleo ya walimu huku zikiwa ni mamlaka ya kushughulikia mashauri ya nidhamu ya walimu pamoja na rufaa za walimu zinazotokana na maamuzi ya mashauri yanayoamuliwa na Wakuu wa Shule.

Kiongozi huyo aliendelea kufafanua kuwa kuwa kutokana na majukumu hayo ambayo mengi yanahusu haki za walimu, watumishi wa TSC wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa, na hivyo wanapaswa kujiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na maadili ya utumishi wao ikiwemo rushwa.

“Kuna baadhi ya watumishi katika Mkoa huu wa Songwe wanatuhumiwa kwa kutengeneza mazingira ya rushwa kwa walimu. Kama mwalimu amekuja ofisini kwako anahitaji huduma alafu unaanza kumzungusha zungusha lazima atahisi unahitaji atoe chochote ndipo umhudumie. Rais ametuamini na kutupa dhamana hii kubwa, kamwe hatupaswi kwenda kinyume na matarajio na iamni aliyotupa,” alisisitiza kiongozi huyo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Momba, Juma Seleman alieleza kuwa Wilaya ya Momba ina Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Momba na Halmashauri ya Mji Tunduma. Wlaya hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 6275 ambapo kilometa za mraba 5856 ni za Halmashauri ya Wilaya ya Momba na 419 ni za Halmashauri ya Mji Tunduma. Aidha, wilaya hiyo inaundwa na jumla ya Kata 29 ambapo Kata 14 zipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba na kata l5 zipo katika Halmashaurj ya Mji Tunduma.

Halmashauri ya Wilaya ya Momba ina jumla shule za msingi 93 zenye walimu 689 na shule za sekondari 14 zenye walimu 201 huku Halmashauri ya Mji Tunduma ikiwa na shule za msingi 49 zenye walimu 507 na shule za sekondari 14 zenye walimu 243 wanaohudumiwa na TSC kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu mafanikio ya Ofisi ya TSC Momba katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, Seleman alisema kuwa ofisi hiyo imefanikiwa kupandisha vyeo walimu 635 ambapo katika idadi hiyo walimu 405 ni wa shule za msingi na 230 ni wa shule za sekondari.

Aliongeza kuwa ofisi yake imepatiwa pikipiki ambayo imekuwa msaada mkubwa katika kusafiri kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine pamoja na kufanya ziara mbalimbali shuleni kwa ajili ya kutoa elimu na kutatua kero na malalamiko ya walimu.

Alihitimisha kwa kusema kuwa nidhamu ya walimu wilayani hapo inaendelea kuimarika tofauti na siku za nyuma ambapo baadhi yao hususan wanaofanya kazi katika maeneo ya vijijini walikuwa wanajihusisha na ulevi wakati wa saa za kazi kitu ambao kilisababisha ofisi hiyo kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Katika ziara hiyo Katibu wa Tume aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Maadili na Nidhamu ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Robert Lwikolea pamoja na maafisa wengine.