Dodoma

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo elekezi ya wajumbe wa Kamati za Wilaya za Kanda ya Kaskazini na Kusini ikiwa ni hitimisho la kufanya mafunzo ya wajumbe hao katika Wilaya 139 za Tanzania Bara.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Wilala ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 ndizo zenye mamlaka ya kuamua masuala ya Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku mbili, Aprili 5 hadi 6, 2022 jijini Dodoma yalifunguliwa na Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba ambaye alisisitiza wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha wanatenda haki katika kuamua masuala mbalimbali ya walimu.

Alifafanua kuwa kumekuwa na  rufaa mbalimbali zinazokatwa na walimu kupinga maamuzi yaliyofanywa na Kamati  za Wilaya ambazo baadhi ya rufaa hizo zinaonekana kutozingatia taratibu kitu ambacho kinasababisha Tume Makao Makuu kubatilisha uamuzi uliofanyika ngazi ya Wilaya.

“Nawaomba sana ndugu Wajumbe wa Kamati za Tume za Wilaya, tuzingatie sana Sheria, Kanuni na Taratibu katika utoaji maamuzi kwa mashauri mbalimbali ya nidhamu kwa Walimu na pia ni vema kujua na kuzingatia kuwa wakati mwingine yanawasilishwa mashauri ya nidhamu ambayo hayana mashiko mbele ya Tume. Tuwe makini sana katika maamuzi yetu kama Kamati na tutende haki kwa Walimu wetu,” alisema Prof. Komba.