KAMATI ZA TSC ZATAKIWA KUSAIDIA WALIMU KUTATUA CHANGAMOTO ZAO
Inaelezwa kuwa moja ya changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma wakiwemo Walimu ni kukosa nafasi ya kusikilizwa na viongozi wao hasa pale wanapokabiliwa na changamoto binafsi kitu ambacho kinawasababishia msongo wa mawazo, kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, kukata tamaa na hatimaye kujikuta wakiingia kwenye makosa ya kinidhamu.
Kutokana na hilo, watendaji wenye dhamana ya kusimamia walimu wametakiwa kuelekeza nguvu zao katika kuwasikiliza walimu na kusaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili badala ya kukaa na kusubiri watende makosa ya kinidhamu ili wawachukulie hatua.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Grace Magembe wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya Wajumbe wa Kamati za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) za Wilaya kutoka Kanda ya Kaskazini na Kusini yaliyofanyika kwa siku mbili, Aprili 5 na 6, 2022 jijini Dodoma.
Dkt. Magembe alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuwasaidia walimu kwa kuwawekea mazingira mazuri ili waweze kutoa huduma bora kwa wanafunzi, hivyo watendaji wenye dhamana ya kuwasimamia hawanabudi kuelekeza nguvu zao katika kutatua changamoto walimu.
“Moja ya changamoto tulizonazo serikalini ni viongozi wenye dhamana ya kusimamia watumishi kutotaka kuwasikiliza. Yaani unakuta mwalimu ana shida anahangaika lakini akifika kwa kiongozi wake hasikilizwi badala yake ni kufokewa na kufukuzwa. Jambo hili linafanya watumishi kuwa na msongo wa mawazo, kukata tamaa na mwisho anaingia kwenye makosa ya kinidhamu na hatimaye anafukuzwa kazi, alisema Dkt. Magembe.
Alisema kuwa pamoja na kwamba Sheria, Kanuni na Taratibu zipo na ni lazima zizingatiwe, ni muhimu pia wenye dhamani kutumia utu, hekima na busara ili kuwasaidia walimu kutoingia kwenye makosa ya kinidhamu badala ya kukaa na kusubiri wafanye makosa ili wawachukulie hatua.
“Ninyi TSC mmepewa dhamana kubwa kushughulikia masuala ya utumishi wa walimu, wasikilizeni walimu na wasaidieni kutatua changamoto zao. Kuna wengine unaweza kukuta wamechanganyikiwa kabisa na wamekata tamaa lakini kumbe ukiwasikiliza utakuta tatizo ni dogo tu, unakwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri unamshauri mnamsaidia walimu mambo yakwenda vizuri. Kutafuta ufumbuzi wa changamoto za walimu ndiyo wajibu wenu,” alisema.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuboresha elimu ikiwemo kujenga madarasa zaidi ya 15,000, kuajiri walimu zaidi ya 6,900, kupandisha madaraja walimu 126,346 na kuwabadilishia kazi/cheo walimu 11,363, hivyo Kamati hizo nazo zina wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo kwa kutekeleleza wajibu wao kwa ufanisi.
Dkt. Magembe alifafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa vizuri hivyo ni lazima TSC ihakikishe kwamba walimu wanatulia kwenye vituo vyao vya kazi na wanafanya kazi wakiwa na amani na utulivu badala kuondoka vituoni kwenda kuhangaikia masuala yao ya kiutumishi.
Alisema TSC inatakiwa kuwa daraja kati ya walimu na ofisi mbalimbali za serikali zinazoshughulikia walimu na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kila mwalimu anayewasilisha shida yake TSC aweze kupatiwa majibu kwa wakati.
“Tunataka kila mwalimu awe na uhakika kuwa akiwa na jambo lolote linahusu utumishi wake akilifikisha TSC litafuatiliwa kikamilifu na kupatiwa ufumbuzi, hivyo hakuna haja kwa yeye kuondoka kituo chake cha kazi kwa ajili ya ufuatiliaji. Ni lazima msaidie kutetea maslahi ya walimu na kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa kwa haraka,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa Mamlaka ya Kamati za Wilaya yaliyoainishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 yanahitaji watu wa adilifu na wanaosimamia haki bila kuogopa kwa kuwa yanahusisha kuamua hatma za ajira za walimu pamoja na maendeleo yao, hivyo wasipokuwa waadilifu walimu wataumia.
“Ninaamimi ninyi ni waadilifu ndio mana mmeteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati hizi. Sheria imewapa mamlaka ya kuamua hatima ya ajira ya mwalimu, mnaweza kutoa adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuza kazi, kuamua mwalimu gani apande daraja na nani asipande, nk. Msipokuwa waadilifu hamtaweza kusimamia na kufanya maamuzi kwa haki na matokeo yake mtawaumiza walimu pamoja na wanaowategemea,” alisema.
Akitoa neno la kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba alieleza kuwa TAMISEMI imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na TSC kitu ambacho kimesaidia changamoto mbalimbali za tume hiyo kupatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, Prof. Komba alieleza kuwa pamoja na jitihada hizo kumekuwa na changamoto kwa upande wa ofisi za halmashauri ambazo zimekuwa ni kero kwa TSC na hivyo kuiomba TAMISEMI itoe maelekezo kwa wahusika ili ufumbuzi upatikane.
Alieleza kuwa moja ya changamoto hizo ni kitendo cha baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kukataa kwa makusudi kutekeleza uamuzi unaotolewa na tume ngazi ya wilaya kwa mashauri ya nidhamu ya walimu au TSC makao makuu kwa rufaa za walimu kitu ambacho ni ukiukwaji wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015.
“TSC ndiyo iliyopewa mamlaka ya kushughulikia nidhamu kwa walimu lakini cha kushangaza TSC inatoa uamuzi kwamba mwalimu hana hatia hivyo arudishwe kazini lakini unakuta mkurugenzi hataki kumrudisha na mwalimu anahangaika tu mtaani. Kwa kweli jabo hili ni baya na linakiuka haki ya mtumishi,” alisema.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa changamoto nyingine ni waajiri kuwasimamishia mishahara au kuwaondoa kwenye orodha ya mishahara walimu hata kabla ya tuhuma zinazowakabili kufikishwa TSC na shauri kufunguliwa kama sheria inavyoelekeza kitu ambacho kimesababisha walimu kukosa haki yao ya kupata mshahara kwa mujibu wa taratibu.
“Changamoto ya tatu ndugu mgeni rasmi ni baadhi ya wajumbe wa kamati za TSC Wilaya hususan Katibu Tawala wa Wilaya na Afisa Elimu kutohudhuria wenyewe kwenye vikao vya Kamati na badala yake wanatuma wawakilishi. Unajua Mjumbe wote ameteuliwa kwa majina na sio kwa vyeo na wamekula kiapo cha kutekeleza majukumu hayo, kutuma mwakilishi sio sawa. Hilo nalo tunaomba mtusaidie kulitolea maelekezo,” alisema Prof. Komba.
Awali, Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alisema mafunzo hayo yamehudhuriwa na wajumbe 103 kutoka Wilaya za Kanda ya Kaskazini na Kusini ambapo wilaya hizo zinakamilisha idadi ya wilaya zote 139 kupata mafunzo ya Kamati.
Pia, aliwapongeza wajumbe wa kamati hizo kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na welidi licha ya kuwa kutopata mafunzo elekezi tangu walipoteuliwa katika nafasi hizo.
“Ndugu mgeni rasmi, wajumbe hawa waliteuliwa mwezi Mei, 2021 na katika kipindi chote wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa weledi licha ya kuwa tulikuwa hatujakutana nao hivi kuwapatia mafunzo elekezi. Nawapongeza kwani wamekuwa wakisoma sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo tumekuwa tukiwatumia katika kutekeleza majukumu yao,” alisema Nkwama.