Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Karibu

Jacobs Mwambegele photo
Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele
Mwenyekiti wa Tume

: uchaguzi@nec.go.tz

: +255 26 2962345-8

UJUMBE WA MWENYEKITI KWENYE TOVUTI YA TUME

Natumia fursa hii kuwakaribisha wadau wa Uchaguzi kwenye Tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Idara Huru inayojitegemea iliyoanzishwa chini ya Ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977.

Majukumu ya Tume yameainishwa katika Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo ni kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara.

Majukumu mengine ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais  na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara, kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya Uchaguzi wa Wabunge; na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.

Jukumu lingine kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume inalo jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo; na kuteua na kutangaza Wabunge na Madiwani Wanawake wa Viti Maalum.

Tovuti hii ni njia muhimu kwa Tume huwasiliana moja kwa moja na wadau wa Uchaguzi, ambapo wadau watapata taarifa mbalimbali za Tume, miongozo na majibu ya maswali ya wadau kuhusu masuala ya uchaguzi ikiwemo Sheria, Kanuni, Miongozo, taratibu na maelekezo yote yanayohusu masuala ya uchaguzi, majimbo ya uchaguzi na kata, matokeo ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na idadi ya wapiga kura walioandikishwa. Aidha, mtaweza kufuatilia akaunti za mitandao ya kijamii za Tume kupitia viunganishi vinavyopatikana chini ya Tovuti hii.

Tunawakaribisha ili muweze kupitia maudhui ya Tovuti yetu, kuwashirikisha wadau wengine na kurejesha mapendekezo, ushauri, maoni na maswali kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa mfumo wa uchaguzi unaoaminika na unaohakikisha chaguzi huru na haki, kwa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa chaguzi kwa mujibu wa sheria na kulinda demokrasia kwa manufaa ya wananchi, vyama vya siasa, wagombea na Taifa la Tanzania kwa ujumla.

Karibuni sana.

 

Mhe. Jaji (R) Jacobs C. Mwambegele

MWENYEKITI

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI