Watumishi wa Tume wachangia damu, wafanya usafi Kituo cha Afya Makole kuadhimisha Wiki ya Utumishi
Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo tarehe 22 Juni, 2023, wamechangia chupa 14 za damu na kufanya usafi wa mazingira katika kituo cha Afya Makole kilichopo jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma nchini ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 16-23 juni.
Watumishi hao wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Raslimali Watu Bw. Leonard Tumua kwanza walifanya usafi wa mazingira kwa kufyeka majani na kukusanya takataka katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho, na kufuatiwa na zoezi la kutoa damu.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kutoa damu, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole Dkt.Revocatus Bartazar amewashukuru watumishi hao kwa kuchangia kiasi hicho cha damu kwani mahitaji ya damu katika kituo hicho kwa akina mama wanaojifungua ni makubwa.
Amesema kwa mwezi akina mama 600 hadi 700 hujifungua katika kituo hicho na mahitaji ya damu ni makubwa kwani asilimia 10 ya akina mama wanaojifungua hukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua.
Amesema sababu kubwa inayopelekea akina mama wanaojifungua kupoteza maisha ni kupoteza damu nyingi baada ya kujifungua.
“Sababu kubwa inayopelekea vifo vya akina mama wanaojifungua nchini Tanzania ni kutoka damu nyingi baada ya kujifungua,” amesema Dkt Bartazar.
Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vifo vitokanavyo na uzazi vinatokana na damu kutoka nyingi baada ya kujifungua hivyo njia ya kupunguza vifo vya aina hiyo ni kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu kama walivyofanya watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Amesema mama aliyepoteza damu nyingi kutokana na kujifungua akipata chupa moja inamsaidia kuweza kurudisha uhai wake, hivyo kwa watumishi hao kuchangia chupa 14 wameweza kuokoa uhai wa akina mama 14 watakaohitaji damu .
Naye Mratibu wa Kitengo cha Damu Salama wa Kituo hicho cha Afya Bw.Jerome Felician Marando amewapongeza watumishi wa NEC kwa kuchangia chupa 14 za damu kwani amesema kiasi hicho ni kikubwa kwani mara nyingi wanapofanya mazoezi ya kuhamasisha watu kuchangia damu wanapata chupa 5 au 6 hivyo kupata chupa 14 ni kitu kikubwa sana kwa mahitaji ya Kituo cha Afya Makole.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Bi. Felister Ishuza amesema shughuli ya usafi na kuchangia damu iliyofanywa na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 16-23 juni.