Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura Kata ya Kinyika watakiwa kuepuka kuvuruga uchaguzi

Imewekwa: 29 Aug, 2023
Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura Kata ya Kinyika watakiwa kuepuka kuvuruga uchaguzi

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Makete Bw. William Makufwe amewataka wasimamizi wa vituo vya kupigia kura katika Kata ya Kinyika kuelewa mafunzo na kuyazingatia watakayofundishwa bila ya kukosea ili kuepuka kuvuruga Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata hiyo unaofanyika Julai 13, 2023.

Bw. Makufwe ameyasema hayo wakati wa kufungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura vya Kata ya Kinyika ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani wa kata hiyo.

Amesema kuwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura ndio kiina cha uchaguzi na ndio wanaohitimisha mchakato wote wa uchaguzi siku ya kupiga kura, hivyo iwapo watafanya ndivyo sivyo watakuwa wameharibu mchakato wote wa uchaguzi huo mdogo.

“Tumefanya mambo mengi kabla ya siku ya leo na tutafanya mengi kabla ya siku ya uchaguzi lakini ninyi wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura ndio mtakaohitimisha maandalizi yote yaliyofanyika kuelekea siku ya uchaguzi” alisema Bw. Makufwe na kuongeza kuwa:

“Kwa hiyo nyinyi msipoelewa mafunzo haya, mkikosea au mkifanya ndivyo sivyo katika kutekeleza majukumu yenu na uchaguzi ukavurugika maana yake maandalizi yote tuliyoyafanya yanakuwa hayana maana yoyote.”

Alisema wanachotakiwa kufanya ni kuwa wasikivu, wadadisi na wazingatie mafunzo watakayopewa ili kutekeleza kwa usahihi yale wanayotakiwa kufanywa siku ya uchaguzi.

Mbali na hilo, Bw. Makufwe aliwataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika Kata ya Kinyika kuwahudumia wapiga kura kwenye vituo kwa weledi, uadilifu na kutumia kauli nzuri ili kufanikisha uchaguzi huo.

Aliwataka wasimamizi hao kuepuka makosa katika kutekeleza majukumu yao na hakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa usahihi kwani kuharibika kwa mchakato wa uchaguzi siku ya kuoiga kura kutasababisha kushindwa kutoa matokeo.

Hivyo aliwataka kuzingatia maadili ya kazi yao na wasichukulie wepesi majukumu yao kwa uzoefu walionao bali kwa kuzingatia mambo watakayofundishwa katika mafunzo hayo.

Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata ya Kinyika unafanyika kutokana na kufariki kwa diwani wa kata hiyo na kata hiyo inaungana na kata nyingine 12 zinazofanya uchaguzi huu mdogo unaotarajiwa kufanyika Siku ya Alhamisi tarehe 13 Julai, 2023.