Wasimamizi wa Uchaguzi waaswa kutofanya kazi kwa mazoea.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoka katika Kata zinazotaraji kufanya uchaguzi mdogo wa udiwani Desemba 17, 2022 kutofanya kazi ya uchaguzi kwa mazoea, badala yake wazingatie sheria, kanuni za uchaguzi pamoja na maelekezo ya Tume katika utendaji wao.
Tume pia imewataka wasimamizi wa nchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha wanavishirikisha Vyama vyote vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi ili kurahisha utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Magdalena Rwebangira wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Mhe.Rwebangira amesema Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha, hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, ni vyema mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea”,alisema Mhe. Rwebangira.
Aidha amewataka kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, na kwamba katika utendaji wa majukumu yao wanapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume na kuongeza kua jambo hilo lisiishie katika mafunzo na nadharia bali ionekane kufuatiwa katika kutenda.
“Sanjari na hilo nawaasa kukumbuka kuvishirikisha Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia sana utekelezaji wa majukumu yenu,”alisema Mhe.Rwebangira.
Wasimamizi hao wametakiwa kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vizuri maeneo ambayo chaguzi utaendeshwa ikiwemo hali ya miundombinu ya kufika katika Kata na hasa Vituo vya kupigia kura.
“Mfanye utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani,”alisema Mhe. Rwebangira.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Magdalena Rwebangira pia amewataka wasimamizi hao kuhakikisha kuwa wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana kuacha undugu au upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.
Alisema jambo muhimu wanalotakiwa kuzingatia Wasimamizi hao wa uchaguzi ni kujiamini, kufanya kazi kwa weredi na kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili ya uchaguzi pamoja na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume.
Aidha Mjumbe wa Tume hiyo ya uchaguzi, aliwasisitizia wasimamizi hao wa uchaguzi kuhakikisha wanafanya utambuzi wa vituo vya uchaguzi mapema kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Stephen Elisante, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema uchaguzi huo mdogo wa udiwani utafanyika katika Kata 12 za Tanzania Bara ila waliopo katika mafunzo hayo Mkoani Morogoro ni kutoka katika Kata sita za Vibaoni – Halmashauri ya Mji wa Handeni, Lukozi – Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Majohe - Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mnyanjani - Halmashauri ya Jiji la Tanga na Dunda - Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
Mapema kabla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo watendaji w uchaguzi hao walikula kiapo cha kutunza siri na kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vyao vya siasa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Mhe. Japhet Bwire Manyama.