Wapiga Kura 114,647 walioandikishwa kushiriki Uchaguzi Mdogo Jimbo la Amani na Kata Sita za Tanzania Bara
Wapiga Kura 114,647 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani Mkoa wa Mjini, Zanzibar na Kata saba za Tanzania Bara tarehe 17 Desemba, 2022.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 17 Desemba, 2022 na kusema kuwa vituo vituo 289 vya kupigia kura vitatumika.
“Tume imekamilisha maandalizi muhimu ikiwemo usambazaji wa vifaa vya uchaguzi na mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi katika ngazi ya vituo vya kupigia kura” alisema Jaji wa Rufaa Mwambegele.
Jaji wa Rufaa Mwambelegele amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya siasa na wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani, Mkoa wa Mjini, Zanzibar na Uchaguzi wa Udiwani katika Kata saba za Tanzania Bara.
Mbali na jimbo la Amani pia uchaguzi huo mdogo utashirikisha, Kata za Majohe (Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam), Mndumbwe (Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba), Njombe Mjini (Halmashauri ya Mji wa Njombe), Dunda (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mwamalili (Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga), Mnyanjani (Halmashauri ya Jiji la Tanga) na Vibaoni (Halmashauri ya Wilaya ya Handeni).
Aidha, amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye jimbo na kata zinazofanya uchaguzi huo.
Jaji wa Rufaa Mwambegele amesema Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.
Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika jimbo ya Amani na Kata saba za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua Mbunge na madiwani wanaowataka.
Amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zimekamilika tarehe 16 Desemba, 2022 saa 12:00 jioni hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.
Aidha Jaji Rufaa Mwambegele amevikumbusha vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi wa huo, kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura.
“Pili upigaji kura utafanyika katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni”alisema Jaji Rufaa Mwambegele na kuongeza:
“Watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Amani Wilaya ya Mjini Zanzibar ni wale tu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na wana kadi za mpiga kura” alisema Jaji wa Rufaa Mwambegele. Aidha Jaji wa Rufaa Mwambegele alisema
“Kwa upande wa uchaguzi mdogo wa madiwani watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wana kadi zao za mpiga kura. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala”.
Amevitaja vitambulisho mbadala kuwa ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura anapokwenda kupiga kura. Aidha majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
Jaji wa Rufaa Mwambegele amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nuktanundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze kupiga kura wenyewe.
Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
Amewakumbusha wapiga kura kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020 yaliyokubaliwa na wahusika wote vikiwemo vyama vya siasa, kuwa wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura, hivyo Tume imewashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura. Jumla ya vyama vya siasa 16 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo ambapo Tume imevipongeza vyama hivyo na wagombea wao kwa kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huu mdogo wa Ubunge na Udiwani.