Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kuwepo ofisini muda wote kesho tarehe 25 Agosti 2020

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kuwepo ofisini muda wote kesho tarehe 25 Agosti 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kuwepo kwenye ofisi zao kesho wakati wote wa kupokea fomu za uteuzi kutoka kwa wagombea ubunge na udiwani kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni na iwapo hawatakuwepo ofisini kwa muda huo Tume itachukua hatua kali dhidi yao.

Hayo yamesemwa leo tarehe 24 Agosti mwaka 2020 na Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Rufaa (Mst.) Semistocles Kaijage wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya kupokea fomu za uteuzi na uteuzi wa wagombea kesho tarehe 25 Agosti 2020.

Jaji Kaijage alisema kesho tarehe 25 Agosti, 2020, Tume itafanya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani nchi nzima.

Alisema uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais utafanyika katika ofisi za Tume zilizopo eneo la Njedengwa jijini Dodoma na uteuzi wa wagombea ubunge utafanyika katika ofisi za wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo na udiwani katika ofisi za wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata.

“Hadi hivi leo, wagombea wa vyama vya siasa 17 vyenye usajili wa kudumu wamechukua fomu za uteuzi wa kiti cha Rais na makamu wa Rais. Kwa upande wa ubunge na udiwani, Tume inaendelea kukusanya taarifa za waliochukua fomu baada ya kupendekezwa na vyama vya siasa.”alisema Jaji Kaijage.

Alifafanua kuwa kesho tarehe 25 Agosti, 2020 ndiyo siku ya uteuzi na kwamba baada ya zoezi la uteuzi, fomu zitabandikwa katika mbao za matangazo za ofisi iliyohusika na uteuzi.

Jaji Kaijage alisema kwa mujibu wa kanuni ya 29 ya kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020 na kanuni ya 27 ya ya kanuni za Uchaguzi wa Madiwani za mwaka 2020, fomu hizo zitawekwa eneo la wazi hadi saa 10 kamili jioni tarehe 26 Agosti, 2020, ambapo wagombea watapata nafasi ya kuweka pingamizi.

Aliongeza kuwa wengine wanaoruhusiwa kuweka pingamizi ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Tume inaelekeza na inawasisitiza Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata kuwepo kwenye Ofisi zao kesho wakati wote kuanzia saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni. Kitendo cha kutokuwepo ofisini katika muda huo kitapelekea Tume kuchukua hatua kali dhidi ya watendaji wa majimbo na kata husika.”alisema Jaji Kaijage.

Kwa upande wa kampeni za uchaguzi, Jaji Kaijage alisema kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi kampeni za uchaguzi zinatarajiwa kuanza tarehe 26 Agosti, 2020 hadi saa 12 jioni tarehe 27 Oktoba 2020, ikiwa ni siku moja kabla ya Siku ya uchaguzi yaani tarehe 28 Agosti 2020.

Alisema kwa upande wa Tanzania Zanzibar, kampeni zitahitimishwa tarehe 26 Oktoba, 2020 ili kupisha upigaji kura wa awali na kwamba Tume inawakumbusha wahusika wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kutii, kuheshimu na kuzingatia Maadili, Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa, yakiwemo makatazo mbalimbali yaliyomo katika Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020.

Jaji Kaijage alivikumbusha vyama vya siasa kuzingatia maelekezo yaliyomo katika Maadili ya Uchaguzi hasa katika eneo la kuzitumia kamati za maadili kutatua migogoro na malalamiko yatakayojitokeza.

Alisema Tume kwa upande wake itaendelea kuzingatia Katiba, Sheria, kanuni za uchaguzi na maelekezo yaliyomo katika Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020.