Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa wakati wa uchaguzi

Imewekwa: 29 Aug, 2023
Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa wakati wa uchaguzi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka Masimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yamesema na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst. Thomas Mihayo wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi hao wa uchaguzi yanayofanyika Mjini Iringa, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika kata 14 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai mwaka 2023.

Alisema iwapo kuna mambo hayahitaji kuwashirikisha wadau hao wasiwashirikishe na wala wasishinikizwe kuwashirikisha na kama yapo mambo ambayo wanapaswa kuwashirikisha basi ni lazima wawashirikishe ili kurahisisha majukumu yao.

Jaji Mst. Mihayo aliongeza kwa kuwataka wasimamizi hao wa uchaguzi kufuata na kuzingatia hatua na taratibu za kisheria katika kutekeleza majukumu yao kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi na hupunguza malalamiko katika uchaguzi.

“Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama si kuondoa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi”, alisema Jaji Mst. Mihayo na kuongeza:

“Jambo muhimu mnalotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kufanya kazi kwa weledi na kwamba katika utendaji wa majukumu yenu, mnapaswa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi mdogo”.

Aliwasisitiza wasimamizi hao wa uchaguzi kuzingatia masuala muhimu ikiwa ni pamoja na kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri unaoruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

Jaji Mst. Mihayo aliwataka wasimamizi hao kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana waachane na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

“Kuhakikisha vifaa vya uchaguzi mnavyovipokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema. Kuhakikisha siku ya uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kinafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo utahitajika ushauri kuhusiana na masuala ya uchaguzi uliopo.”, alisema Jaji Mst. Mihayo.

Mafunzo haya ya siku tatu kwa Masimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi lengo lake ni kuwajengea uwezo na kuwakumbusha wajibu na majukumu yao wakati wote wa uchaguzi na yanafanyika pia katika mkoa wa Tanga kwa watendaji wengine wanaotarajia kusimamia uchaguzi mdogo kutoka katika halmashauri nyingine.