Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka 2020

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka 2020

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Rufaa Mst. Semistocles Kaijage amewasisitiza wasimamizi wa uchaguzi kuwa wana jukumu la kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu.

Jaji Kaijage ameyasema hayo leo tarehe 24 Julai, 2020 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi cha Wasimamizi wa Uchaguzi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka huu.

Alisema ili kufanikisha hilo wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa kuhakikisha wanaepuka dosari zinazoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi na kuathiri shughuli za uchaguzi huo.

Hivyo aliwataka waandae mipango mizuri ya uendeshaji wa uchaguzi na wayaelewe vyema mazingira yanayoweza kuathiri ufanisi wa uchaguzi huo.

“Vilevile mnalo jukumu la kuwasimamia watendaji wa uchaguzi waliopo chini yenu ili nao wakatekelezea majukumu yao kwa weledi na umakini mkubwa”, alisema Jaji Kaijage.

Aliwataka wasimamizi hao wa uchaguzi kuyasoma na kuyaelewa maadili ya uchaguzi na kuyazingatia katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi kwani wao ndio wenyeviti wa kamati za maadili katika majimbo wanayoyasimamia na wanapaswa kusimamia utekelezaji wake.

“Kanuni za Maadili zinaeleza kuwa katika kipindi chote cha uteuzi wa wagombea, upigaji kura na katika hatua ya mchakato wa uchaguzi, watendaji wa Tume watatakiwa wakati wote kuwepo katika maeneo yao ya kazi. Ninawasisitiza kuzingatia hili kwani uzoefu unaonesha baadhi ya watendaji wa uchaguzi katika chaguzi zilizopita wamekuwa wakikiuka maadili haya hali iliyopelekea kuwepo kwa malalamiko. Vilevile nisisite kuwasiliana na Tume kwa jambo lolote lile ambalo mnadhani linahitaji ufafanuzi.”, alisisitiza Jaji Kaijage.

Kuhusu watendaji wa uchaguzi, Jaji Kaijage alisema Tume imewateua Waratibu wa Uchaguzi 28, Wasimamizi wa Uchaguzi 194, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo 742 na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata 7,912.

Aliwaeleza wasimamizi hao wa uchaguzi kuwa Tume inatambua kuwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi watafanya kazi chini yao, hivyo wanatakiwa kuhakikisha wanawapangia majukumu watendaji hao ili kuwe na ufanisi katika zoezi la uchaguzi na kuhakikisha wanaandaa utaratibu utakawezesha watendaji hao kuyaelewa majukumu na kuyatekeleza kwa mujibu wa Sheria na maelekezo ya Tume.

Jaji Kaijage aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha asasi 79 zilizopewa vibali vya kutazama uchaguzi na asasi 245 zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura watakaofanya kazi maeneo yao, wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Mwongozo wa Watazamaji na Mwongozo wa Utoaji Elimu ya Mpiga Kura iliotolewa na Tume.

Kuhusu mawakala wa vyama vya siasa, Jaji Kaijage aliwakumbusha kuwa mawakala hao ni muhimu kwani husaidia kudhihirisha uwazi katika uchaguzi, hivyo wahakikishe wanazingatia maelekezo ya Tume kuhusiana na utambulisho wao na kuzingatia utaratibu wa kuwaapisha ili kuepusha malalamiko yanayoweza kujitokeza.

Tume imetangaza kuwa kuanzia tarehe 5 Agosti mwaka huu itaanza kutoa fumo za uteuzi hadi Agosti 25 na kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 26 Agosti hadi 27 Oktoba na siku ya uchaguzi ni tarehe 28 Oktoba mwaka huu.