Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yatoa vibali kwa Asasi tatu kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi wa Udiwani wa Desemba 17, 2022

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yatoa vibali kwa Asasi tatu kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi wa Udiwani wa Desemba 17, 2022

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa Taasisi au Asasi tatu za Kiraia kwenye Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata tatu za Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Nassoro Shemzigwa vibali hivyo vimetolewa baada ya kikao cha Tume kilichokaa tarehe 25 Novemba mwaka 2022.

“Baada ya uhakika na upembuzi wa maombi yaliyopekelewa, Tume katika kikao chake cha tarehe 25 Novemba, 2022 iliridhia Taasisi au Asasi zifuatazo kupewa vibali kwa ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura” alisema Bw. Shemzigwa.

Alizitaja taasisi au asasi hizo kuwa ni Tanzania Building Future Organization (TABUFO) ya Mkoa wa Mtwara iliyopewa kibali kutoa elimu katika Kata ya Mndumbwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

Taasisi au Asasi nyingine iliyopewa kibali ni Tanzania Peace, Legal Aid and Justice Centre (PLAJC) ya Mkoa wa Dodoma iliyopewa kibali kutoa Elimu katika Kata ya Dabalo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

Aliongeza kuwa Taasisi au Asasi ya Umbrella of Women and Disabled Organization (UWODO) ya Mjini Njombe ilipewa kibali cha kutoa Elimu kwenye Kata ya Njombe Mjini katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inazikumbusha Taasisi au Asasi hizo kuwa zitawajibika kujigharamia katika zoezi la kutoa Elimu ya Mpiga Kura” alibainisha Bw. Shemzigwa.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 4 C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume imepewa mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia Taasisi au Asasi na watu wanaotaka kutoa elimu hiyo.

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani Tanzania Zanzibar na Udiwani katika Kata 12 za Tanzania Bara unatarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba mwaka 2022.