Tume yatoa uamuzi wa rufaa 46 za wagombea udiwani na kuwarejesha wagombea 24 kwenye uchaguzi
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezipitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa 46 za wagombea udiwani waliowasilisha rufaa zao Tume kutoka kata mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa kwa umma jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Septemba, 2020 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Dkt. Wilson Mahera Charles amesema kati ya rufaa hizo Tume imekubali rufaa 24 na kuwarejesha wagombea katika orodha ya wagombea Udiwani.
Ametaja kata ambazo wagombea wake wamerejeshwa kuwa ni kata ya Dunda (Bagamoyo), Mtwivila (Iringa Mjini), Kikilo (Kondoa), Makurumla (Ubungo), Hezya (Vwawa), Makorongoni (Iringa Mjini), Bwawani (Arumeru Magharibi), Jinjimili (Magu), Kimnyaki (Arumeru Magharibi).
Dkt. Charles ametaja kata nyingine kuwa ni kata ya Lemanyata (Arumeru Magharibi), Mkwawa (Iringa Mjini), Kisarawe II (Kigamboni), Makurumla (Ubungo), Mbabala (Dodoma Mjini), Mpanda Hotel (Mpanda Mjini), Lusungo (Kyela), Same (Same), Maisaka (Babati Mjini), Makuburi (Ubungo), Kibada (Kigamboni), Maore (Same Mjini) na rufaa tatu kutoka Kata ya Mshindo (Iringa Mjini).
Katika hatua nyingine, Dkt. Charles amesema Tume imekataa rufaa 13 za wagombea ambao hawakuteuliwa kutoka kwenye Kata za Kawajense (Mpanda), Mjini Chirombola (Ulanga), Mabokweni (Tanga Mjini).
Amezitaja kata nyingine kuwa ni Chanika (Karagwe), Mwamala (Manonga), Kiomboi (Iramba Magharibi), Mwasenkwa (Mbeya Mjini), Old Iramba (Iramba Magharibi), Magara (Babati Vijijini), Arri (Babati Vijijini), Chapwa (Tunduma) na rufaa mbili kutoka Kata ya Kibamba (Kibamba).
“Tume imekataa rufaa 9 za kupinga walioteuliwa kutoka kwenye Kata za Nonde (Mbeya Mjini), Mwagata (Iringa Mjini), Mabibo (Ubungo), Mkimbizi (Iringa Mjini), Kipanga (Sikonge), Nsoho (Mbeya Mjini), Ilemi (Mbeya Mjini), Bagara (Babati Vijijini) na Nkinga (Manonga)”, amesema Dkt. Charles.
Amesema idadi hiyo ya rufaa 46 inafanya jumla ya rufaa za wagombea Ubunge zilizofanyiwa uamuzi na Tume kufikia 113 na za wagombea Udiwani 149.
Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kila siku na kwamba wahusika wa rufaa hizo watajulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa Tume.