Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yatoa fomu za uteuzi kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais Imewekwa: August 06, 2020

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yatoa fomu za uteuzi kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais Imewekwa: August 06, 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa fomu za uteuzi kwa mgombea wa kiti cha Rais kutoka Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Ofisi za Tume zilizopo Njedengwa jijini Dodoma.

Dkt. Magufuli amefika ofisini hapo akiwa ameambata na Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgombea wa kiti cha Makamu wa Rais, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Bashiru Ally na viongozi wengine wa chama.

Baada ya kufika kwenye ofisi za Tume, Dkt. Magufuli alipokelewa na kamati ya mapokezi kwenda kusaini kitabu na ndipo akapokelewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Wilson Charles ambaye alimpeleka hadi kwenye ukumbi wa utoaji wa fomu.

Kabla ya utaoji fomu Mwenyekiti wa Tume Jaji Uchaguzi Jaji wa Rufaa (Mst.) Semistocles Kaijage alimkumbusha mgombea kuwa siku ya uteuzi anatakiwa kurejesha fomu hizo na baada ya Tume kujiridhisha kuwa anayo sifa itamteua.

“Itakapofika siku ya Uteuzi tarehe 25 Agosti, 2020 mtarejesha fomu zenu hapa Tume, na Tume baada ya kujiridhisha kuwa mnazo sifa itawateua”alisema Jaji Kaijage.

Akiungumza wakati wa kumkaribisha mwenyekiti, Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Charles alieleza taratibu mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa ikiwemo kuzingatia sifa za wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, fedha za dhamana na kusaini tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi.

Dkt. Magufuli ni mgombea wa tatu kuchukua fomu za uteuzi baada ya jana tarehe 5 Agosti, 2020 wagombea kutoka Chama cha AAFP, Seif Maalim Seif na mgombea wa Chama cha Demokrati (DP) Philipp John Fumbo kuchukua fomu za uteuzi.