Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yatangaza Siku ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yatangaza Siku ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza siku ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara kuwa ni siku ya Jumatano ya tarehe 28 Oktoba mwaka huu 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Rufaa (Mst.) Semistocles Kaijage, amesema Uteuzi wa Wagombea Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, Ubunge, na Udiwani utafanyika tarehe 25 Agosti, 2020 na kampeni za Uchaguzi zitaanza tarehe 26 Agosti, 2020 hadi 27 Oktoba mwaka huu wa 2020.

 

Alisema Tume imetoa taarifa hiyo chini ya Ibara ya 41(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na vifungu vya 35B (1), (37) (1) (a) na 46 (1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 48 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

 

“Tume inapenda kuutarifu Umma kuwa Ratiba ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara itakuwa kama ifuatavyo.Uteuzi wa Wagombea Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, Ubunge, na Udiwani utafanyika tarehe 25 Agosti, 2020, kampeni za Uchaguzi zitaanza tarehe 26 Agosti, 2020 hadi 27 Oktoba mwaka huu wa 2020 na Siku ya Uchaguzi itakuwa tarehe 28 Oktoba, 2020”alisema Jaji Rufaa (Mst) Kaijage.

 

Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara kwa mwaka huu wa 2020, unakuja baada ya uchaguzi kama huo uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka 2015.