Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yashiriki Maonesho ya Sherehe za Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yashiriki Maonesho ya Sherehe za Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mara ya kwanza inashiriki Maonesho ya Sherehe za Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayofanyika kwenye viwanja vya Maisara Unguja kwa kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi wanaotembelea banda la Tume.

Maonesho hayo yameanza tarehe 1 Januari mwaka 2023 hadi siku ya kilele cha Sherehe za Mapinduzi tarehe 12 Januari mwaka 2023 huku taasisi mbalimbali za Serikali zikishiriki maonesho hayo ambapo Kaulimbiu ya sherehe inasema Mapinduzi Yetu Ndio Amani Yetu, Tuyalinde kwa Maendeleo Yetu.

Katika maonesho hayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa Elimu ya Mpiga kura kwa kukutana na wananchi ana kwa ana na kuwapa elimu, kujibu maswali mbalimbali ya wadau wa Uchaguzi kuhusu masuala ya kiuchaguzi na kugawa vipeperushi kwa wananchi wanaotembelea banda la Tume.

Hata hivyo, Sherehe za mwaka huu za Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazonogeshwa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi, hazitafanyika baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kufuta sherehe hizo.

Akizungumzia suala hilo Dkt. Mwinyi alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizo za miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Shilingi Milioni 450 zitatumika kujenga madarasa, kuongeza madawati, maabara na huduma nyingine za sekta ya elimu visiwani Zanzibar.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inashiriki kwenye maonesho hayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya Kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 kinachoipa mamlaka Tume kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima na kuratibu watu wanaotaka kutoa elimu hiyo.