Tume yapokea rufaa 557 kutoka kwa wagombea ubunge na udiwani Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepokea rufaa 557 kutoka kwa wagombea ubunge na udiwani kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu wa 2020.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Rufaa Mst. Semistocles Kaijage wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Amesema rufaa hizo zinatokana na baadhi ya wagombea ubunge na udiwani kutoridhika na maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi na kwamba baada ya kupokea rufaa hizo itaanza kuzifanyika kazi leo na itajitahidi kuzitolea uamuzi mapema kwa kadri itakavyowezekana.
Jaji Kaijage amesema baada ya kukamilika kwa uteuzi wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa sasa Tume ipo katika hatua ya kupokea rufaa kutoka majimboni kwa ajili ya wagombea ubunge na kutoka katika kata mbalimbali kwa ajili ya wagombea udiwani.
“Hadi hivi sasa Tume imepokea jumla ya Rufaa zipatazo 557 ambazo itaanza kuzifanyika kazi leo na itajitahidi kuzitolea uamuzi mapema kwa kadri itakavyowezekana.” amesema Jaji Kaijage.
Amefafanua kuwa Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imeweka masharti ya wajibu wa kila mtu kufuata na kutii Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano na imeainisha haki ya kila mtu, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria, kuchukua hatua za kisheria kwa madhumuni ya kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi.
Jaji Kaijage amefafanua kuwa malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hizo, yanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu na kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza wagombea wa Vyama vya Siasa mbalimbali ambao wamedai haki zao kwa kufuata taratibu za kisheria na za kikanuni katika kuweka pingamizi mbalimbali na hatimaye kukata rufaa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume itazishughulikia rufaa hizo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa.”, amesema na kuongeza kuwa:
Kwa ujumla Sheria za uchaguzi na kanuni zake zimeweka masharti, taratibu na hatua za kuchukua panapokuwa na malalamiko ama ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi. Aidha, Sheria hizo zimeainisha mamlaka za kushughulikia malalamiko husika. Taratibu hizo zimebainishwa katika hatua mbalimbali za uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea hadi kutangaza matokeo. Hivyo ni wajibu wa wagombea na Vyama vyao vya Siasa kujua haki zao, mamlaka husika na hatua za kuchukua pale ambapo hawajaridhika na jambo, katika kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.”
Jaji Kaijage amevipongeza Vyama vya Siasa na wagombea ambao tayari wameanza kampeni za uchaguzi na wanaendelea nazo, katika maeneo mbalimbali na kwamba Tume inaendelea kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wagombea kufanya kampeni za kistaarabu na zinazozingatia maadili ya uchaguzi ambayo wahusika wake wakuu ni Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Vyama vya Siasa na wagombea.
Mwenyekiti huyo wa NEC amesisitiza kuwa Tume ilipokutana na Vyama vya Siasa katika vikao mbalimbali ilivikumbusha vyama hivyo na serikali kuzingatia makubaliano ya pande zote, kuyafuata na kuyatekeleza maadili ya uchaguzi katika kipindi chote cha kampeni.
Hivyo amesema katika uchaguzi wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba, 2020, Tume haitarajii kuona Vyama vya Siasa vikilalamika kuhusu ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi, badala ya kuchukua hatua stakihi za kisheria kwenye mamlaka husika.
Amebainisha hatua hizo kuwa ni pamoja na kuzitumia kamati za maadili, ambazo zimepewa mamlaka ya kushughulikia malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi husasan katika kipindi cha kampeni.
Jaji Kaijage amekumbusha kuwa kamati za maadili tayari zimeundwa kuanzia ngazi ya Kata kwa uchaguzi wa Madiwani, ngazi ya Jimbo kwa uchaguzi wa Wabunge na ngazi ya Taifa kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Makamu wa Rais na Kamati ya Rufaa kwa wale ambao hawataridhika na maamuzi ya kamati nyingine.
“Kamati hizo zimepewa uwezo wa kuyashughulikia malalamiko ya ukikwaji wa maadili ya uchaguzi. Aidha, mlalamikaji asiporidhika na maamuzi ya kamati katika ngazi husika anaweza kukata rufaa. Ikumbukwe kuwa wajumbe wa kamati hizo walio wengi ni wawakilishi kutoka kila Chama cha Siasa kilichosimamisha mgombea katika ngazi husika.”, amesema Jaji Kaijage na kuongeza kuwa:
“Ni muhumu kwa wadau wa uchaguzi, vikiwemo Vyama vya Siasa, wagombea wa nafasi mbalimbali na wananchi kwa ujumla, kutambua kwamba wakati huu ambapo Tume inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, utekelezaji wa sheria nyingine za nchi haujasimama. Hivyo kila mwananchi anashauriwa kujihadhari na maneno ama vitendo ambavyo vinatishia amani na utulivu uliopo nchini kwa kisingizio cha uchaguzi.”
Jaji Kaijage amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kusoma kitabu cha Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombea ya Mwaka 2020. Kitabu hicho kina ufafanuzi wa mchakato wote wa uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea, pingamizi, rufaa, kampeni na maadili, mawakala wa Vyama vya Siasa, hatua za upigaji kura hadi kutangaza matokeo.