Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yapewa mafunzo juu ya ukatili dhidi ya wanawake katika siasa

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yapewa mafunzo juu ya ukatili dhidi ya wanawake katika siasa

Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imepatiwa mafunzo juu ya ukatili unaoathiri wanawake kujihusisha na siasa.

Mafunzo hayo ambayo ni ya siku mbili yanayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitivo cha Sayansi ya Jamii na uongozi (PSPA) chini ya mradi wa Uwezeshaji wa Mwanamke katika Siasa na Uongozi kwa kushirikiana na UN-Women yamelenga katika kutoa uelewa kwa watendaji jinsi ya kushughulikia masuala mbalimbali yanayojitokeza kwa wanawake wenye nia ya kuingia katika siasa.

 

Akifungua mafunzo hayo muwakilishi kutoka UN Women, Bi. Julia Broussard amesema uzuiaji wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ni suala mtambuka na linatakiwa kushughulikiwa kwa kuzingatia ushirikiano wa taasisi mbalimbali na jamii kwa ujumla.

 

Bi Julia alieleza kuwa ni muhimu kubadilika kwa kuangalia njia sahihi, mbinu na jinsi ya kusaidia jamii ili kuhakikisha vitendo hivyo vya ukatili vinazuiwa.

“Wapo wanawake wanaotamani kuingia katika siasa ila kwa ajili ya jinsi yao na wakikumbuka ukatili unaofanyika kwa wanawake katika siasa huogopa kushiriki katika siasa” Alisema. Bi. Julia.

 

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Makamu Mkuu wa Chuo –Tafiti, Prof. Bernadetha Killiani ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mradi huo alisema, mradi huu ulianzishwa kwa lengo la kuwatayarisha wanawake wenye nia ya kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2020.

 

Mafunzo hayo yalitolewa kwa wanawake mia saba thelathini na tatu (733) na kati ya hao wanawake waliochukua fomu walikuwa mia tatu arobaini na tisa (349) sawa na asilimia arobaini na nane (48%) ya wanawake waliotaka kugombea nafasi katika siasa.

 

Prof. Kiliani amesema wanawake wengi wamekumbana na vitendo vya unyanyasaji kiasi cha kuwakatisha tamaa katika safari zao za siasa. Unyanyasaji wa kijinsia huanza katika ngazi ya familia, kwa kudharau uwezo wa wanawake wa uongozi katika siasa.

 

Hivyo, ameziomba taasisi husika zinazoshughulikia masuala ya siasa kuangalia namna itakavyosaidia jamii kuelewa uwezo wa mwanamke katika Nyanja ya siasa.

 

Prof Kiliani alitoa mfano kati ya majimbo mia mbili sitini na nne (264) yaliyopo ni majimbo ishirini na sita tu (26) ambayo yanaongozwa na wanawake, akieleza kwamba hali hiyo inaonesha kama kungekuwa hakuna viti maalumu kwa wanawake basi idadi ya wanawake bungeni ingekuwa ni ndogo sana.

 

Aidha, alieleza kuwa kadri idadi ya wanawake inavyoongezeka katika siasa ndivyo idadi ya ukatili inavyoongezeka.Kitu kinachosukuma ukatili dhidi ya unyanyasaji kwa wanawake hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine hata hivyo yapo mambo ya msingi ambayo jamii zote hukubaliana kuwa ni unyanyasaji wa kijinsia.

 

Aidha, katika mafunzo hayo imeelezwa kuwa ili kuweza kuondoa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ni muhimu jamii kufasiri kwa pamoja maana ya jinsi,jinsia, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake.

 

Ukatili wa kijinsia kwa wanawake katika siasa unaweza kuwa katika kesi za udhalilishaji wa kingono, kubakwa, matishio ya kingono au kutengenezewa picha za udhalilishaji. Wapo wanawake wanao pigwa na kutekwa kwa ajili ya kujihusisha na siasa.

 

Mafunzo haya ya kukataa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake tayari yameshayatoa pia kwa makundi na taasisi mbalimbali za kisiasa.