Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yaongeza siku tatu wasimamizi wa uchaguzi kuapisha mawakala wa vyama vya siasa kwa ajili ya uchaguzi

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Tume yaongeza siku tatu wasimamizi wa uchaguzi kuapisha mawakala wa vyama vya siasa kwa ajili ya uchaguzi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeongeza siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo yote nchini kuapisha mawakala wa vyama vya saisa kwa ajili ya siku ya uchaguzi tarehe 28 Oktoba, 2020.

Uamuzi huo umetangazwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo Dkt. Wilson Mahera Charles wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Dkt. Charles amesema siku hizo tatu ni kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2020 na uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha Tume kilichokaa siku ya jumatano tarehe 21 Oktoba, 2020.

Amesema Tume imefanya uamuzi huo kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa na Kifungu cha 57 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 58 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Ameongeza kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na changamoto ya kutofikika kwa urahisi kutokana na jiografia na hivyo kuwa vigumu kwa wasimamizi wa uchaguzi kuwafikia na kuwaapisha mawakala hao kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Dkt. Charles alivitaka vyama vya saisa vipeleke orodha ya mawakala wao na viwe vimewapanga mawakala hao katika vituo vya kupigia kura na kuweka anuani au namba ya simu ya kila wakala husika.

“Lakini tunaviasa vyama vya saisa kupeleka mawakala kwa utaratibu unaokubalika na iwapo vitapeleka mawakala wasiohusika au kuwapeleka kwenye eneo ambalo sio lao na bila kufuata utaratibu wanaweza kujikuta wako matatani”, amesema Dkt. Charles na kuongeza:

“Ila ni matarajio ya Tume kuwa hii kazi ya kuwaapisha mawakala wa vyama vya siasa litaendelea kufanyika kwa utaratibu mzuri ambapo wasimamizi wa uchaguzi watatenga maeneo katika jimbo ambayo yanafikika kiurahisi”

Dkt. Charles amevitaka vyam vya siasa kufuata utaratibu wa kisheria na kwa mujibu wa maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea vitapata fursa kwa mawakala wao kuapishwa.

Amefafanua kuwa mawakala wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na Urais.