Tume yamtangaza Dkt. Magufuli kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Oktoba 28, 2020
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imemtangaza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura nyingi halali kuliko wagombea wengine na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM katika Uchaguzi wa Rais uliofanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu.
Hayo yametangazwa jijini Dar es Salaam tarehe 30 Oktoba, 2020 na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Rufaa Mst. Semistocles Kaijage baada ya kukamilika kwa utangazaji wa matokeo ya kura za Rais katika majimbo yote 264.
Jaji Kaijage amesema mgombea huyo wa CCM amepata kura 12,516,252 kati ya kura halali 14,830,195 zilizopigwa na idadi halisi ya waliopiga kura 15,091,950 kati ya wapiga kura 29,754,699 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapig Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na walioandikishwa kwenye Daftaria la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Amewataja wagombea wengine kutoka vyama 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Rais na kura walizopata kwenye mabano kuwa ni Mahona Leopold Lucas wa NRA (80,787), Shibuda John Paul wa chama ADA TADEA (33,086) na Muttamwega Bhatt Mgaywa wa chama cha SAU (14,922).
Amewataja wagombea wengine ni Cecilia Augustino Mmanga wa Chama cha Demokrasia Makini aliyepata kura 14, 556, Maganja Yeremia Kulwa wa Chama cha NCCR Mageuzi amepata kura 19,969, Lipumba Ibrahim Haruna wa Chama cha CUF amepata kura 72,885.
Jaji Kaijage ameongeza kuwa mgombea Philipo John Fumbo kutoka Chama cha DP amepata kura 8,283, Membe Bernard Kamillius wa Chama cha ACT-Wazalendo amepata kura 81,129, Queen Cuthbert Sendiga wa Chama cha ADC amepata kura 7,627.
“Mgombea Twalid Ibrahim Kadege wa Chama cha UPDP amepata kura 6,194, Rungwe Hashim Spunda wa Chama cha CHAUMA amepata kura 32,878, Mazrui Khalfani Mohamed wa Chama cha UMD amepata kura 3,721, Seif Maalim Seif wa Chama cha AAFP amepata kura 4,635 na Lissu Tundu Antiphas Mughwai wa Chama cha CHADEMA amepata kura 1,933,271”, amesema Jaji Kaijage.
Baada ya kutangaza matokeo hayo mawakala 12 wa vyama vya siasa kati ya mawakala wa vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Rais walisaini Fomu Namba 27, kati ya mawakala 13 waliokuwepo wakati wa kutangazwa matokeo hayo.
Jaji Kaijage amesema ametangaza matokeo hayo kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 38 (1), Ibara ya 41 (6) na Ibara ya 47 (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 35 (f) (8) na Kifungu cha 35 (h) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania.
Mbali na kura halali zilizohesabiswa, Jaji Kaijage amesema idadi ya kura zilizokataliwa ni kura 261,755.
Amesema baada ya kutangaza matokeo hayo ya uchaguzi wa Rais, siku ya Jumapili Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatoa hati ya ushindi kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais walioshinda.