Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yafanya Uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi

Imewekwa: 23 May, 2023
Tume yafanya Uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya uteuzi wa madiwani wanawake wa viti maalum kujaza nafasi wazi za madiwani katika Halmashauri tatu za Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima, uteuzi huo umefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitaarifu kuwepo kwa nafasi wazi.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, aliitaarifu Tume kuhusu kuhusu uwepo wa nafasi wazi za Madiwani Wanawake wa Viti Maalum katika Halmashauri tatu za Tanzania Bara. Nafasi hizo zimetokana na vifo vya madiwani wanawake wa Viti Maalum wa Kata husika.” alisema Bw. Kailima.

Aliwataja madiwani walioteuliwa kuwa ni Ndugu Sina Jamaldin Nyanga (CCM) kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Ndugu Mary Muhjimy Kombe (CCM) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Ndugu Mashavu Juma Barakabitse  (CCM) kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Aliongeza kuwa uteuzi huo ulifanywa na Tume katika kikao chake cha tarehe 08 Mei, 2023 kwa kuzingatia kifungu cha 86A cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kikisomwa pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287 na kifunga cha 19 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288.