Tume yafanya uamuzi wa rufaa 616 zilizowasilishwa na wagombea ubunge na udiwani
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya uamuzi wa rufaa 616 za wagombea ubunge na udiwani katika Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 28, 2020.
Hayo yamsemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo Dkt. Wilson Mahera Charlse wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu uchambuzi na uamua wa rufaa za wagombea wa ubunge na Udiwani.
Amesema hadi kufikia jana tarehe 17 Septemba, 2020, baada ya kupitia kumbukumbu zote za rufaa zilizowasilishwa, Tume imepokea jumla ya rufaa 616 zikiwemo za ubunge rufaa 160, udiwani rufaa 456, malalamiko 25 na rufaa zilizojirudia 44.
“Katika rufaa 160 za ubunge zilizoamuliwa na Tume matokeo yake ni wagombea waliorejeshwa ni 66, wagombea ambao hawakurejeshwa ni 32, rufaa zilizokataliwa za kuomba kuenguliwa wagombea 57 na rufaa zilizojirudia ni 5.
Dkt. Charles ameongeza kuwa baada ya Tume kupitia rufaa zilizowasilishwa kutoka katika majimbo hayo, imerejesha wagombea 3 waliokuwa wameenguliwa katika majimbo ya Namtumbo, Bukene na Kavuu.
Amesema kutokana na uamuzi huo majimbo hayo matatu yataendelea na kampeni na uchaguzi utafanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
“Baada ya kupitia na kuamua rufaa mbalimbali, Tume imekubali rufaa tatu (3) na kuwaengua wagombea katika majimbo matatu. Kwa matokeo hayo wabunge waliopita bila kupingwa ni 18”, amesema Dkt. Charles na kuongeza kuwa:
“Pia, Tume imepokea taarifa ya kujitoa kwa wagombea wa Ubunge kwenye Majimbo ya Chalinze na Madaba, hivyo kubakia wagombea pekee ambao wanakuwa wamepita bila kupingwa”.
Amesema kufuatia kumalizika kwa kipindi cha pingamizi na rufaa, wagombea waliopita bila kupingwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ni 20.
Amefafanua kuwa Tume itawatangaza katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa sheria.