Tume yafanya uamuzi wa rufaa 50 za wagombea ubunge na udiwani
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imezipitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa 50 za wagombea ubunge na udiwani ambapo kati ya rufaa hizo 4 ni za wagombea ubunge na 46 ni za wagombea udiwani.
Haya yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles wakati akitangaza uamuzi wa kikao cha Tume kilichokutana jana tareje 12 Septemba.
Amesema kati ya rufaa hizo 50, Tume imekataa rufaa zote 4 za wagombea ubunge kutoka jimbo la Babati Mjini ambazo ni za wagombea ambao uteuzi wao ulitenguliwa, hivyo wagombea hao wanaendelea kutokuwa kwenye orodha ya wagombea.
“Aidha, Tume imezipitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa 46 za wagombea udiwani, imekubali rufaa 25 na kuwarejesha wagombea Udiwani katika orodha ya wagombea Udiwani.”, amesema Dkt. Charles.
Ametaka kata ambazo rufaa hizo zimetoka kuwa ni kata ya Changaa (Kondoa), Kichonda (Liwale), Kisima (Same Magharibi), Kibada (Kigamboni), Utende (Katavi), Myamba (Same Mashariki), Buswelu (Ilemela), Kiseke (Ilemela), Kimochi (Moshi Vijijini), Kikilo (Kondoa).
Kata nyingine ni Bereko (Kondoa), Isanga (Maswa Magharibi), Kirumba (Ilemela), Liwale Mjini (Liwale), Mshewe (Mbeya Vijijini), Nar (Babati Vijijini), Namiungo (Tunduru Kaskazini), Kimbiji (Kigamboni), Chitete (Ileje), Dunda (Bagamoyo), Kimambi (Liwale), Ludewa (Ludewa), Mwabusalu (Kisesa), Konje (Handeni Mjini) na kata ya Makurumla (Ubungo).
Dkt. Charlse ameongeza kuwa, Tume pia imekataa rufaa 12 za wagombea udiwani ambao hawakuteuliwa kutoka kwenye Kata za Mwayaya (Buhigwe), Bwakira Chini (Morogoro Kusini), Lalago (Maswa Mashariki), Duga (Tanga Mjini), Makurumla (Ubungo), na kata ya Ngoywa (Sikonge).
“Kata nyingine ni Isyesye (Mbeya Mjini), Iwambi (Mbeya Mjini), Oltrumet (Arumeru Magharibi), Iyunga (Mbeya Mjini), Bumilayanga (Mafinga Mjini) na Kahangara (Magu).”, amesema Dkt. Charles.
Katika hatua nyingine, Dkt. Charles amesema Tume pia imekataa rufaa 9 za kupinga wagombea Udiwani walioteuliwa kutoka kwenye Kata za Maendeleo (Mbeya Mjini), Forest (Mbeya Mjini), Kashaulili (Mpanda Mjini), Isanga (Mbeya Mjini), Mbalizi Road (Mbeya Mjini), Itende (Mbeya Mjini), Sinde (Mbeya Mjini), Boma (Mafinga Mjini) na Makuro (Singida Kaskazini).
Amefafanua kuwa idadi hiyo ya rufaa za wagombea ubunge zilizofanyiwa uamuzi na Tume zimefikia rufaa 117 na za wagombea udiwani zimefikia rufaa 195.
Dkt. Charles amesema kuwa Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kila siku. Wahusika wa rufaa hizo watajulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa Tume.