Tume yaamua rufaa 67 za wagombea ubunge na udiwani na kuwarejesha wagombea 45 kwenye uchaguzi
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezipitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa 67 za wagombea ubunge na udiwani na kuwarejesha wagombea 45 wa ubunge na diwani katika majimbo na kata mbalimbali nchini.
Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 10 Septemba, 2020 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Dkt. Wilson Mahera Charles kufuatia kikao cha tume kilichaokaa jana tarehe 9 Septemba, 2020 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Charles amesema kati ya rufaa 67 zilizotolewa uamuzi, rufaa 22 ni za wagombea ubunge na rufaa 45 ni za wagombea udiwani kutoka majimbo na kata mbalimbali nchini.
Amesema katika kikao hicho Tume imekubali rufaa 19 na kuwarejesha wagombea husika katika orodha ya wagombea kutoka kwenye majimbo ya Tunduru Kaskazini, Mbeya Vijijini, Songea Mjini, Karagwe, Ulanga, Chemba, Tanga, Kibamba, Nyasa, Same Mashariki, Buhigwe, Mufindi Kusini, Muheza, Tabora Kaskazini, Ubungo (2) na Kigamboni (3).
“Tume pia imekataa rufaa 3 za kupinga walioteuliwa. Rufaa hizo ni kutoka kwenye majimbo ya Kalambo, Kigamboni na Muheza”, amesema Dkt. Charles.
Kwa upande wa rufaa za udiwani, Dkt. Charles amesema Tume imezipitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa 45 za madiwani na kuzikubali rufaa 26 na kuwarejesha wagombea husika katika orodha ya wagombea Udiwani.
Dkt. Charles amezitaja rufaa hizo kuwa zimetoka kwenye kata za Kingolwira (Morogoro Mjini), Kilakala (Morogoro Mjini), Bwera (Chato), Bugene (Karagwe Mjini), Babati (Babati Mjini), Mzingani (Tanga), Bukindo (Ukerewe), Kihanga (Karagwe), Central (Tanga Mjini), Muriti (Ukerewe),
Ametaja kata nyingine kuwa ni Namagondo (Ukerewe), Kakukuru (Ukerewe), Bukindo (Ukerewe), Mindu (Morogoro Mjini), Kitangiri (Ilemela), Ilemela (Ilemela), Buzuruga (Ilemela), Magaoni (Tanga),
Kata nyingine ni Uwanja wa Taifa (Morogoro Mjini), Kerege (Bagamoyo), Chemchem (Kondoa Mjini), Tungi (Morogoro Mjini), Ndama (Karagwe), Mbuyuni (Morogoro Mjini), Kiwanja cha Ndege (Morogoro Mjini), Igurwa (Karagwe Mjini).
“Tume imekataa rufaa 16 za wagombea ambao hawakuteuliwa. Rufaa hizo ni kutoka kwenye Kata za Ilangala (Ukerewe), Kandawe (Magu), Mazimbu (Morogoro Mjini), Msindo (Same Magharibi), Kiomoni (Tanga Mjini)”, amesema Dkt. Charles na kuongeza kata nyingine kuwa ni:
Magaoni (Tanga Mjini), Usagara (Tanga Mjini), Kayanga (Ukerewe), Namilembe (Ukerewe), Nakatunguru (Ukerewe), Bwiro (Ukerewe), Kihanga (Karagwe), Kisegese (Mkuranga), Mnyajani (Tanga Mjini) na Rufaa mbili kutoka Kata ya Ngoma (Ukerewe).”
Amesema kuwa Tume pia imekataa rufaa 3 za kupinga walioteuliwa. Rufaa hizo ni kutoka kwenye Kata ya Ipwani (Mbarali), Ilemela (Ilemela) na Kichangani (Ulanga).
Kufuatia uamuzi wa rufaa hizo 67, Dkt. Charles amesema idadi hiyo inafanya jumla ya rufaa za wagombea ubunge zilizofanyiwa uamuzi na Tume hadi sasa kufikia 111 na za wagombea Udiwani 45.
Amesema Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo. Wahusika wa rufaa hizo wameanza kujulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa Tume.