Rais Dkt. Magufuli azindua Jengo la Utawala la Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dododma
Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua jengo la utawala la Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma huku akiviomba vyama vya siasa kufanya kampeni kiustaarabu na kwa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ili kuufanya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu kuwa uchaguzi ’special’.
Akizunguamza kabla ya uzinduzi huo Rais Dkt. Magufuli aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wakati wa kampeni wafanye kampeni kwa kumtanguliza Mungu na kwa kujenga umoja wa kitaifa na kunadi sera ili wananchi wawapime kwa sera zao na sio matusi.
”Mimi naamini tukienda hivyo uchaguzi huu utakuwa mzuri sana na utakuwa huru.Na niviombe kwa sababu ninaamini vyama vyote vitaendesha kampeni kwa ustaarabu, basi tukawe wavumilivu.Lakini niviombe vyombo vya kusimamia haki ikiwemo vyombo vya dola, tuvumilieni kidogo, tusitumie nguvu mahali ambapo hapahitajiki kutumia nguvu” alisema Dkt. Magufuli na kuongeza:
”Lakini niwaombe na nyinyi wanasiasa msiwachokoze wale walinda amani, msiwafanye wakatumia nguvu mahali ambapo nyinyi mmewataka watumie nguvu”.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage alisema uzinduzi huo unaashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Tume jijini Dodoma na kwamba shughuli zote za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2020 zinatarajiwa kufanyika kwenye jengo hilo.
Alisema kwa muda mrefu Tume imekuwa ikitumia majengo ya kupanga katika jiji la Dar es Salaam kuendesha shughuli zake, hali iliyoleta changamoto za kiutendaji kutokana na ofisi hizo kuwa finyu na kuwa katika maeneo matatu tofauti.
Hivyo Jaji Kaijage amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira yake ya kuhakikisha Tume inapata fedha kwa ajili ya kujenga ofisi zake za kudumu.
Alisema mradi huo ulipangwa kutekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya Shilingi Bilioni 13.3, hata hivyo kutokana na changamoto za utekelezaji ikiwa ni pamoja na mapungufu katika usanifu na kuchelewa kukamilika kwa mradi kwa mujibu wa muda uliokubaliwa kwenye mkataba, kulifanyika uamuzi wa kuvunja mkataba na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) na kuingia mkataba mpya na SUMA- JKT kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha utekelezaji wa mradi.
“Tangu kuingia Mkataba kati ya Tume na SUMA JKT, mradi umekuwa ukitekelezwa kwa kasi na hadi sasa mradi huu umekamilika kwa wastani wa asilimia 89 (Jengo la Ofisi ambalo utalizindua hivi punde limekamilika kwa asilimia 97, Ghala asilimia 92, Jengo la Kutangazia matokeo asilimia 79 na kazi za nje - external works asilimia 88). Aidha, tarehe 15 Julai, 2020 SUMA JKT alifanya makabidhiano ya awali ya jengo la ofisi na hivyo kuiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuanza kutumia ofisi hizo”, alisema Jaji Kaijage.
Jaji Kaijage aliongeza kuwa ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo na hasa jengo la kutangazia matokeo, kutakuwa na mahitaji mbalimbali kama vile samani za ofisi na vifaa vya kutangazia matokeo ili kuwezesha utangazaji wa matokeo.
Jaji Kaijage aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushiriki kwa karibu na kushauri katika utekelezaji wa mradi huo, Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano ambao waliutoa katika utekelezaji wa mradi huo huku akitoa shukrani zake kwa SUMA JKT chini ya uongozi wa Meja Jenerali Charles Mbuge, makamanda, askari na vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa ustadi, umahiri, kasi, weledi, uzalendo na nidhamu katika utekelezaji wa mradi huu.
”Vilevile, kwa niaba ya Tume nitoe shukrani za kipekee kwa Chuo Kikuu cha Ardhi kwa kusimamia kwa umakini na weledi ujenzi wa jengo hili”alisema Jaji Kaijage.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama, alitoa shukrani kwa Rais Dkt Magufuli kwa kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni heshima kwake na matokeo chanya kwa serikali ya awamu ya tano.
Kwa upande wake Mkuu wa JKT Menja General Charles Mbuge alisema kwa sasa jengo la ofisi lililozinduliwa limekamilika kwa asilimia 97, wakati ghala limekamilika kwa asilimia 92, jengo la kutangazia matokeo likikamilika kwa asilimia 79 huku kazi za nje - external works asilimia 88 na kwamba hadi kufikia tarehe 30 Agosti, 2020 karibu mradi wote wa ujenzi wa jengo hilo utakuwa umakamilika.
Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Makatibu na Manaibu Katiba Wakuu na Wakuu wa vikosi vya Ulinzi na Usalama na wananchi wa eneo la Njadengwa ulipo mradi huo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshatangaza ratiba ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambapo uteuzi wa wagombea wa nafasi zote utafanyika Agosti 25 na kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 26 Agosti hadi 27 Oktoba wakati siku ya Uchaguzi itakuwa tarehe 28 Oktoba mwaka huu.