Balozi Mapuri akumbusha malengo ya Kamati ya Uchaguzi ya Elimu ya Mpiga Kura na Asasi za Kiraia
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema lengo la kuunda Kamati ya Uchaguzi ya Elimu ya Mpiga Kura na Asasi za Kiraia ni kuhakiki kuwa elimu ya mpiga kura inayotolewa kwa wapiga kura ni ile iliyokusudiwa na Tume ili iwawezeshe wapiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka wakiwa na taarifa sahihi.
Hayo yamesema na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mjumbe wa Tume Mhe. Balozi Omari Mapuri wakati akifungua kikao cha kamati hiyo jijini Dar es Salaam leo.
Balozi Mapuri amesema kwa sasa Tume inaendelea kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vyombo vya habari yakiwemo magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii ikiwemo mitandao ya kijamii ya Tume.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwaelimisha wapiga kura juu ya mambo ya msingi yatakayowawezesha kutekeleza kwa usahihi jukumu la kupiga kura siku ya uchaguzi tarehe 28 Oktoba, 2020.
“Wapiga kura watapata fursa ya kujua ni nani wanaoruhusiwa kupiga kura, wapi wanaweza kupiga kura, kituo cha kupigia kura, muda wa kupiga kura, mambo muhimu ya kuzingatia mpiga kura awapo kituoni kabla na baada ya kupiga kura na jinsi ya kupiga kura”amesema Balozi Mapuri.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, Tume imeandaa Mkakati wa Habari na Utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura ambao umeainisha njia na mbinu zitakazotumika kutoa taarifa kwa wananchi na kuwahamasisha kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu.
Balozi Mapuri ameongeza kuwa Tume pia imeandaa machapisho mbalimbali ya elimu ya mpiga kura vikiwemo vijitabu, vipeperushi, mabango karatasi na mabango ya kielekroniki ili kuhakikisha kila mwananchi anapata taarifa zitakazomuwezesha kushiriki katika uchaguzi akiwa na taarifa sahihi.
Mbali na Tume kutekeleza hayo, Balozi Mapuri amesema Tume imeshazipatia vibali asasi 245 za kiraia kwa Tanzania Bara na asasi 7 za Tanzania Zanzibar kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura ambapo kati ya hizo asasi 19 zinashughulika na watu wenye ulemavu, asasi 24 zinazoshughulika na wanawake, asasi 33 za vijana na asasi 169 zinazoshughulika na makundi yote.
“Ni imani ya Tume kuwa kwa kushirikiana na asasi zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura, wapiga kura wengi zaidi wataweza kufikiwa”, amesema Balozi Mapuri.
Amesema katika kuhakikisha asasi hizo 245 zinajengewa uwezo, Tume ilizialika na kuzipa mwongozo wa kutoa elimu ya mpiga kura ambapo kati ya asasi hizo ni asasi 228 zilizohudhuria na kupitishwa kwenye mwongozo huo kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu utoaji elimu ya mpiga kura na kuhakikisha elimu inayotolewa ni ile iliyokusudiwa.
Kamati ya Uchaguzi ya Elimu ya Mpiga Kura na Asasi za Kiraia ina wajumbe 16 kutoka vyama vya siasa vya DP, SAU, ADC, CUF, NCCR Mageuzi, UMD na AAFP.Wajumbe wengine ni kutoka Asasi za Kiraia za TAFEYOCO na WISE.
Wajumbe wengine ni kutoka vyama vya watu wenye ulemavu ambavyo ni SHIVYAWATA na CHAWATA na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).