Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Asasi zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura Zanzibar zakumbushwa mambo ya kuzingatia

Imewekwa: 10 Feb, 2023
Asasi zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura Zanzibar zakumbushwa mambo ya kuzingatia

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imezitaka asasi za kiraia zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura Tanzania Zanzibar, kutumia vibali hivyo kutoa elimu hiyo badala ya kuchanganya elimu ya mpiga kura na kampeni za vyama vya siasa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura Bi. Giveness Aswile wakati akifungua mafunzo kwa asasi hizo kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, visiwani Zanzibar.

Amesema elimu ya mpiga kura kimsingi haitakiwi kuegemea upande wowote lakini wakati mwingine asasi inaweza bila kujua ikajikuta inafanya kampeni kutokana na mazingira inayotumia kutolea elimu hiyo.

“Inawezekana hili likajitokeza kutokana na mazingira unayotolea elimu hiyo, kwa mfano unatumia jengo la chama cha siasa au eneo linalofahamika na watu kuwa ni chama fulani”, amesema Bi Aswile na kufafanua kuwa:-

Lengo la maelezo haya ni kuwataka kuwa makini na mambo ambayo nayaweza kuleta sintofahamu bila sababu yoyote ya msingi”

Amewataka wawakilishi wa asasi hizo za kiraia kutotumia kwa ubia vibali walivyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na asasi nyingine yoyote ile na hasa zile ambazo hazikupewa vibali hivyo.

Amefafanua kuwa Tume hiyo inafahamu kuwa baadhi ya asasi zilizopewa vibali wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, zilitumia vibali vyao kwa ubia na asasi nyingine.

Bi. Aswile amebainisha kuwa Tume inaendelea na itaendelea kufuatilia kwa karibu asasi yoyote itakayobainika kukiuka maagizo na maelekezo waliyopewa, na kwamba Tume haitasita kusitisha kibali cha asasi hizo wakati wowote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Thabit Idarous Faina amezikumbusha asasi hizo kuwa zinakwenda kuwapa elimu wananchi wa aina tatu tofauti.

Amebainisha makundi hayo kuwa ni wananchi ambao ni wanachama wa chama cha siasa, mashabiki wa chama cha siasa na wale ambao hana chama chochote cha siasa.

“Kwa hiyo tuwe makini sana wakati tunapokwenda kuwasilisha elimu yetu bila kuwakwaza wale ambao wanakwenda kupata fursa hii ya elimu katika maeneo yao”, amesema Faina.

Wakati akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Habari) Dkt. Cosmas Mwaisobwa amesema lengo la elimu ya mpiga kura ni kuongeza idadi ya wapiga kura watakaokwenda kupiga kura.

Amekumbusha takwimu za wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kuwa kati ya wapiga kura milioni 23 ni wapiga kura takribani milioni 15 walijitokeza kupiga kura ambayo ni idadi ndogo ya wapiga kura.

Hivyo amesisitiza kuwa elimu ya mpiga kura inatakiwa itotelewe ili idadi ya wapiga kura watakaojitokeza kupiga kura iongezeke.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamezungumzia umuhimu wa elimu hiyo na kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutoa mafunzo hayo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Viziwi, Zuberi Ally Haji amesema amefurahi kupata mafunzo hayo kwani yatasaidia watu wenye ulemavu kuelimisha jamii ya watu wenye ulemavu wa uziwi katika Unguja na Pemba.

Amesema baada ya mafunzo hayo watu wenye ulemavu wa uziwi wanategemea kwamba itakapofika siku ya uchaguzi ushiriki wa viziwi utakuwa ni mkubwa sana.