Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Karibu

Ramadhani Kailima photo
Ndg. Ramadhani Kailima
Mkurugenzi wa Uchaguzi (Katibu wa Tume)

: uchaguzi@nec.go.tz

: +255 26 2962345-8

UJUMBE WA MKURUGENZI WA UCHAGUZI

Kwa niaba ya Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wadau wa uchaguzi kwa ushirikiano mkubwa mnaotoa katika kipindi chote ambacho Tume inatekeleza majukumu yake kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Wadau wa uchaguzi ni mhimili muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Tume. Ushiriki wenu katika hatua mbalimbali za mchakato wa uchaguzi unatoa mchango mkubwa kwa Tume katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake zimeipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Aidha, Tume imepewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara, kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.

Mbali na majukumu hayo, Tume pia imepewa mamlaka ya kuteua na kuwatangaza Wabunge na Madiwani Wanawake wa Viti Maalum na kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima; kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.

Mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu haya ya Tume kwa mujibu wa katiba na sheria za uchaguzi, hayawezi kutenganishwa na ushiriki wa kiwango kinachostahili cha wadau wa uchaguzi kama vile vyama vya siasa, wapiga kura, taasisi, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla.

Moja ya njia kuu ya kuhakikisha mafanikio haya yanaimarika zaidi ni kuwasisitiza wadau wa uchaguzi kuzifahamu sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi, miongozo na maelekezo ya Tume na kutekeleza matakwa yake wakati wote wa utekelezaji wa majukumu ya kiuchaguzi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia tovuti na akaunti zake za mitandao ya kijamii inatoa fursa kwa wadau kupata taarifa mbalimbali za Tume, miongozo na majibu ya maswali mbalimbali ya wadau kuhusu masuala ya Tume na Uchaguzi.

Ni matumaini ya Tume kuwa Tovuti hii itawasaidia wadau wa uchaguzi kufahamu sheria na kanuni za uchaguzi, pamoja na miongozo mbalimbali ya Tume na kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za mchakato wa uchaguzi.

Hatua hii, itaimarisha zaidi ujenzi wa demokrasia katika chaguzi zetu na kuifanya nchi yetu iendelee kuwa mfano bora wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Tume ipo tayari muda wote kutoa ushirikiano na miongozo inayohitajika kwa wadau ili waweze kuisaidia Tume kutimiza malengo yake na Taifa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Uchaguzi.

Karibuni sana.

 

Kailima, R. K

MKURUGENZI WA UCHAGUZI