Waziri Bashungwa Akipongeza Chuo cha Taifa cha Ulinzi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb) amekipongeza Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kwa mafanikio waliyoyapata kutokana na kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Chuo cha Taifa cha Ulinzi kimeendelea kufanya kazi kubwa na kuileta heshima nchi yetu.
Pongezi hizo zimetolewa na Mheshimiwa Bashungwa wakati alipofanya ziara yake ya kwanza na ya kawaida Chuoni hapo tangu ateuliwe na Mheshimiwa Rais mnamo tarehe 03 Oktoba, 2022 kuiongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Akiongea na Maafisa na Askari, amesema kuwa Chuo cha NDC kimeendelea kuwa ni alama muhimu kwa Taifa letu. Kwa maana hiyo, Waziri Bashungwa amewataka kuendelea kudumisha nidhamu ambayo ndiyo msingi mkuu kwa mwanajeshi kokote duniani, kuendelea kujifunza kasi ya mabadiliko ya kidunia yanayotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, pamoja na kuwa wabunifu kwa kubuni mbinu mbalimbali ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Aidha, kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kutembelea Chuoni hapo Mheshimiwa Bashungwa amemshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuwa sehemu yao, ili aweze kumsaidia katika jukumu ya kuiongoza Wizara hii nyeti na Muhimu.
Vile vile, Waziri Bashungwa amewahakikishia wanachuo hao kuwa, ataendelea kuwasemea kuhusu changamoto zinazowakabili. Ameongeza kusema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga ustawi wa majeshi yetu.
Naye Mkuu wa Chuo hicho, Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona wakati akitoa taarifa fupi kuhusu Chuo, amesema Chuo Cha Taifa cha Ulinzi kilichoanzishwa tarehe 10 Septemba, 2012 kinayo majukumu ya kuwaleta pamoja maafisa wakuu kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja viongozi waandamizi kutoka Serikalini, kuwaandalia mazingira rafiki ya mafunzo ya ulinzi na usalama, kuwajengea washiriki uelewa wa pamoja, kuandaa mtaala kuhusu usalama na stratejia, kuendesha kozi ndefu zinazojumuisha washiriki kutoka Tanzania na nje ya nchi, pamoja na kozi fupi ambazo ni maalum kwa viongozi hapa nchini.
Aidha, Jenerali Mhona amesema kuwa tangu kuanzishwa kwake, Chuo kimefanikiwa kutoa prestigious Symbol ‘ndc’ kwa Washiriki wa kozi ndefu, kupata usajili na ithibati, kuendesha kozi ndefu zipatazo 11 na kozi fupi idadi 14, Chuo kimeweza kujitangaza ndani na nje ya nchi, kuanzishwa kwa Kitengo cha Utafiti, kupatikana kwa Jengo Kuu na Utawala, kupata mgao wa fedha Bilioni 78 kutoka Serikalini kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mabweni ya kuishi washiriki wa kozi ndefu pamoja na kuwa na Bodi ya Usimamizi wa Chuo.
Chuo cha Taifa cha Ulinzi kilianzishwa kwa lengo la kulisaidia Taifa katika kujenga uwezo wa viongozi wanaohitimu mafunzo hapa wawe na uchambuzi wa kina na wa kimkakati, ili waweze kutatua mambo mbalimbali ya usalama wa Taifa na matatizo yanayotakiwa kushughulikiwa kimkakati.
Aidha, Chuo kilianzishwa kuwaleta pamoja washiriki kutoka taasisi zote za Serikali na sekta binafsi waweze kujadili mambo mbalimbali ya kimkakati, ili wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao watambue kuwa ni kwa kiasi gani matokeo ya maamuzi yao yanaathiri mambo ya kijamii, kiuchumi, mahusiano ya kidiplomasia na siasa za ndani kwa ujumla wake.