SHIRIKIANENI KUHAKIKISHA JUDO INAFANYA VIZURI
service image
29 Dec, 2021

Uongozi mpya wa Chama cha mchezo wa Judo Tanzania (JATA), umetakiwa kushirikiana kwa karibu na wadau wa mchezo huo ili kuhakikisha unafanya vizuri zaidi kitaifa na kimataifa.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 29 Disemba, 2021 na Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Milinde Lutiho Mahona ambaye pia alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya kusimamia uchaguzi wa JATA, punde tu mara baada ya kutangaza uongozi mpya uliochaguliwa kwenye uchaguzi uliofanyika katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

"Mmepewa dhamana ya kuongoza Chama hiki kwa miaka minne sasa kuanzia leo na mmeapa kwa Katiba yenu na Sheria ya BMT, hivyo basi mnatakiwa kushirikiana kwa karibu na wadau wenu waliowachagua kuhakikisha mchezo wa Judo unafanya vizuri zaidi kitaifa na kimataifa", alisema Mahona.

Aidha Mahona pia ameusisitiza uongozi mpya kuzingatia misingi ya Utawala Bora katika utendaji kazi wake, ili kuepusha sintofahamu na migogoro inayoweza kujitokeza katika Chama na kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo wa Judo.

" zingatieni sana misingi ya Utawala Bora, hatutaki kusikia kesho na kesho kutwa kuwa kuna mgogoro ndani chama kwa sababu tu, viongozi mmeshindwa kuendesha chama kwa uwazi, weledi na kutoshirikiana wenyewe kwa wenyewe, mmeshakuwa kitu kimoja sasa ni kusonga mbele kwa maslahi ya mchezo wa Judo na Taifa letu", amesisitiza Mahona.