Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA UJENZI WA BWAWA LA KIDUNDA
MRADI WA UJENZI WA BWAWA LA KIDUNDA

1.0 UTANGULIZI

Mahitaji ya huduma ya majisafi kwa wananchi yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu hali inayosababishwa na ukuaji wa uchumi na uimarikaji wa huduma muhimu za kijamii kwenye eneo husika.

Ongezeko hili la watu, licha ya kuwa na tija katika ukuaji wa Uchumi na upatikanaji na uimarikaji wa huduma ya muhimu za kijamii, husababisha kupungua kwa upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi walio wengi, hususani pale ambapo vyanzo vya maji vinapokuwa vichache kushinda mahitaji.

Mbali na Mikoa mingine, Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, ni moja ya Mikoa ambayo imekuwa ikikumbwa na uhaba wa maji kutokana na kupanuka kwake kunakochangiwa na ongezeko kubwa la watu la mara kwa mara.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, upatikanaji wa maji bado umeegemea katika vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni Mto Ruvu, Mto Wami na Mto Kizinga na Visima virefu vya Kigamboni vilivyoanza kutumika rasmi mwaka 2023.

Kutokana na changamoto hii, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan iliweka mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya majisafi kwa asilimia 95 kufikia mwaka 2025, na asilimia 100 kufikia mwaka 2023 sambamba na mkakati wa Dunia wa maendeleo endelevu 2030.

Hivyo, Serikali iliidhinisha mpango wa kuongeza upatikanaji wa majisafi kwa Dar es Salaam na Pwani kwa kuamua kutenga fedha za kutekeleza mradi mkubwa wa kuhifadhi maji wa Bwawa la Kidunda litakalosaidia kutunza na kusambaza maji kwa wananchi kwa kipindi chote cha mwaka. 

 

1.1 CHIMBUKO LA MRADI

Mradi wa Bwawa la Kidunda ulisanifiwa wakati wa ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu miaka ya 1950, japokuwa kwa kipindi cha awamu zote za Serikali kuanzia ya awamu ya kwanza mpaka awamu ya tano, mradi huu haukuweza kutekelezwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha.

Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira uliokithiri katika chanzo cha Mto Ruvu, kina cha maji cha mto huo kimekuwa kikipungua hasa wakati wa kiangazi, hivyo kusababisha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kukosa kusukuma maji ya kutosha na kuleta changamoto ya huduma ya maji kwa wananchi.

Lakini, kupitia Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mradi huu wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 329 umeanza kutekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za Serikali.

Akihutubia wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa mradi huu mkubwa utawezesha kuwepo kwa uhakika wa maji kwa kipindi chote cha mwaka mzima kwa Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani, kwa kuwa kwa sasa Mikoa hii inategemea maji ya Mto Ruvu ambayo ni asilimia 88 ya maji yote yanayozalishwa kwa ajili ya kuhudumia wakazi wake.

Mwaka 2011, Serikali iliupitisha mradi huu na kuingizia katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa lengo la kufikia dira ya Serikali ya mwaka 2025.

Mradi huu ni muhimu kwa kuwa utasaidia kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wanaotarajiwa kuongezeka na kufikia 11,387,753 kwa mwaka 2032, ambapo mahitaji ya maji yanatabiriwa kufikia lita bilioni 1,028,000,000 kwa siku.

 

1.2 Malengo makuu ya mradi;

  • Kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi kwa kuhakikisha maji katika Mto Ruvu yanapatikana kwa kipindi chote cha mwaka ili kutoa huduma ya majisafi kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Kibaha na mji wa Bagamoyo.
  • Kuwezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa matumizi ya majumbani na viwandani.
  • Kuboresha huduma ya usafirishaji kwa kujenga na kuboresha barabara zinazoelekea eneo la mradi kati ya Kijiji cha Kidunda na Ngerengere.

 

1.3 UTEKELEZAJI WA MRADI

Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi wa kampuni ya Sino Hydro Corporation kutoka China ambaye tayari ameanza utekelezaji wa mradi na kazi inaendelea.

Mradi wa Kidunda utawezesha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini yenye kuzalisha jumla ya lita milioni 466 kwa siku, kuwa na uwezo wa kuzalisha maji katika majira yote ya mwaka na hivyo kuepusha upungufu wa maji katika majira ya kiangazi. Mitambo hii inatoa huduma kwa zaidi ya asilimia 80 ya eneo la huduma la DAWASA.

 

1.4 Ujenzi wa mradi umehusisha utekelezaji wa kazi mbalimbali zikiwemo;

  • Uboreshaji wa barabara kwa kiwango cha changarawe.
  • Ujenzi wa nyumba za muda za Mkandarasi ikiwemo ofisi na sehemu ya kuweka vifaa vya ujenzi.
  • Kufunga Mtambo wa kusaga mawe.
  • Kufunga mtambo wa kuzalisha zege (concrete batching plant).
  • Ujenzi wa barabara ya Ngerengere uliopo katika hatua ya kusafisha, ambapo mpaka sasa takribani kilomita 17 zimeshasafishwa tayari. Takribani asilimia 22 ya urefu wa barabara imefanyiwa usafi.
  • Ujenzi wa njia za umeme kutoka Kidunda kwenda kituo cha kupooza umeme kilichopo Chalinze.  
  • Kazi zinazoendelea katika Bwawa ni ujenzi wa cofferdam (protection dike) na uchimbaji (excavation).

 

1.5 Kazi zinazoendelea kutekelezwa eneo la mradi

  • Kusafisha eneo la barabara kwa ajili ya kuanza ujenzi.
  • Ujenzi wa kingo za Mto (protection dike).
  • Kuchimba eneo la Bwawa (excavation).
  • Kupasua mawe yanayotumika katika ujenzi (Brusting).
  • Kutengeneza tofali zitakazotumika kujengea nyumba za mwajili (Employer’s camps).
  • Kusaga mawe (crushing).

 

Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda unatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu ambapo unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.