Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
VINGUNGUTI NA BUGURUNI WANUFAIKA NA MRADI WA KISASA WA UONDOSHAJI MAJI TAKA
07 May, 2024
VINGUNGUTI NA BUGURUNI WANUFAIKA NA MRADI WA KISASA WA UONDOSHAJI MAJI TAKA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa kisasa wa uondoshaji majitaka kwa kutumia teknolojia ya mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka (Simplified Sewerage System) kwenye maeneo ya makazi holela ya wananchi wa Vingunguti na Buguruni Jijini Dar es Salaam. 

Mfumo huo wa kisasa unatekelezwa na DAWASA kwa kushirikiana na benki ya Dunia kwa lengo la kuboresha usafi wa mazingira kwenye makazi ya wananchi. 

Msimamizi wa mradi Mhandisi Amon Gracephord, amesema kuwa  ni mradi wa tofauti na ambao unasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na utiririshaji hovyo wa majitaka mitaani na katika makazi ya watu.

“Utekelezaji wa mradi huu ni matokeo ya mafanikio ya mradi wa awali ulioleta matokeo chanya kwenye mitaa ya Buguruni na Vingunguti kwa kuweza kukabili uchafuzi wa mazingira na kuokoa wananchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko,” amesema Mhandisi Gracephord. 

“Kwa mradi huu, majitaka yatakuwa yanaondoshwa kutoka majumbani kupitia kwenye mifumo rahisi inayojengwa itakayounganishwa moja kwa moja kwenye vyoo vya wananchi na kuepuesha majitaka kutiririka mitaani,” ameeleza Mhandisi Gracephord. 

Amebainisha kuwa huu ni mradi unaotekelezwa kwenye maeneo 12 ya Mkoa wa Dar es Salaam ambao unahusisha ujenzi wa mtandao wa mabomba kwa urefu wa kilomita 56.5 pamoja na kujenga mitambo minne midogo ya kutibu majitaka  kwenye maeneo ya Sinza, Kinyerezi na Kipawa. 

“Huu ni mfumo rahisi ambao unatuwezesha kulaza bomba katika vina vifupi na kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi sana, na mpaka sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 30 ambapo mwezi wa kumi mwaka huu utakamilika na kuruhusu wananchi kunufaika,” ameeleza. 

Kwa mujibu wa Mhandisi Amon, awali kabla ya mradi huu, wananchi walikuwa wakitumia mifumo ya zamani ya kukusanya majitaka kwenye makaro na kuyasafirsha kwa gharama kubwa. Changamoto kubwa ilikuwa namna ya ufikaji kwenye makazi ya wananchi. 

Amesema pia kuwa kupitia mradi huu, magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yanawakabili wananchi wa maeneo haya yataisha, pia gharama za uondoshaji wa majitaka zitapungua na wananchi watapata unafuu wa kulipa gharama ndogo tofauti na mwanzo. 

Kwa upande wake mnufaika wa mradi Ndugu Isaya Selestine mkazi wa Vingunguti, amesema kuwa kabla ya mradi huu kuanza, hali ya maeneo hayo ilikuwa mbaya sana kwa kuwa hapakuwa na uondoshaji mzuri wa majitaka. 

Ameongeza kuwa DAWASA  imetoa elimu ya usafi wa mazingira ili kusaidia kuboresha vyoo na kuimarisha huduma ya usafi wa mazingira. 

“Hatua hii ni ya muhimu sana kwa jamii yetu maana inatusaidia kuokoa usalama wa afya zetu na niwapongeze na kuwashukuru sana DAWASA kwa mradi huu,” amesema Ndugu Selestine.