MRADI WA UJENZI WA MITAMBO YA KISASA YA KUCHAKATA TAKATOPE
Usafi wa Mazingira ni jambo la muhimu na linalohitaji kupewa kipaumbele katika ustawi wa jamii yoyote ili kuboresha afya na uzima wa wananchi.
Katika kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa na kuboreshwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imebuni na kuanza kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya usafi wa mazingira.
Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa mitambo ya kukusanya na kuchakata majitaka kwenye maeneo mbalimbali yaliyoainishwa.
UTANGULIZI;
Mradi wa ujenzi wa mitambo ya kisasa ni mojawapo ya mradi mkubwa wa kimkakati ambao Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imewekeza fedha ili kutekeleza mradi huu.
Lengo la mradi ni kuboresha huduma ya uondoshaji wa majitaka, pamoja na usimamizi sahihi wa takatope ili kuondoa uwezekano wa jamii kukumbwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu, kichocho na homa za matumbo yenye kuleta athari kubwa ikiwemo vifo.
Mradi huu umekuja kufuatia kukithiri kwa tatizo la muda mrefu la uchafuzi wa mazingira kwenye makazi ya watu, pamoja na changamoto ya uondoshaji wa takatope kutoka kwenye makazi ya watu iliyochangiwa na umbali na gharama kubwa iliyokuwa inatozwa na watoa huduma binafsi.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Mradi ulianza kutekelezwa rasmi katika mwaka wa fedha 2023/24 kupitia mkandarasi wa mradi Kampuni ya Ukandarasi ya Shanxi kutoka China. Kwa sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 20.
Utekelezaji ulizingatia hatua mbalimbali ikiwemo zifuatazo;
- Ujenzi wa mitambo ya kuchakata majitaka inayojengwa kwenye Wilaya zote tano Jijini Dar es Salaam na yenye uwezo wa kuchakata majitaka kwa ujazo tofauti tofauti.
- Mradi unajenga mitambo katika maeneo ya Mabwepande, Kisopwa, Kimbiji, Gezaulole, Vijibweni, Vikunai, Mtoni na Zingiziwa.
- Mtambo wa Mabwepande utakuwa na uwezo wa kuchakata lita 170,000 za majitaka za siku, Kisopwa mtambo utakuwa na uwezo wa kuchakata lita 170,000 kwa siku, Kimbiji 50,000 kwa siku, Gezaulole lita 120,000 kwa siku, Vijibweni lita 50,000 kwa siku, Vikunai lita 120,000 kwa siku, Mtoni lita 50,000 kwa siku na Zingiziwa lita 50,000 kwa siku.
Huu ni mradi wa kimkakati ambao umejengwa kwenye Wilaya zote za Dar es Salaam ikiwemo Kinondoni, Kigamboni, Ilala, Temeke na Ubungo.
Mradi unatekelezwa kwa kuhusisha ujenzi wa mitambo 8 ya kuchakata takatope zinazotoka kwenye makazi ya watu.
Kwa pamoja, mitambo yote nane inauwezo wa kuchakata lita 780,000 za majitaka kwa siku. Mradi umegharimu kiasi cha bilioni 35 na umelenga kunufaisha wakazi 1,700,000 wa maeneo tajwa.