UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI KIGAMBONI – KIMBIJI
UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI KIGAMBONI
Upatikanaji wa huduma ya majisafi ni mojawapo ya kipaumbele muhimu ambacho Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hii ya msingi.
Dhamira hii ya Serikali imedhihirika baada ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika eneo la Kigamboni ambapo mradi mkubwa wa kimkakati wa usambazaji maji umetekelezwa kwa lengo la kunufaisha zaidi ya wananchi 250,000 ambao hawakuwa na huduma ya uhakika.
UTANGULIZI
Mradi wa Maji Kigamboni ni mojawapo ya mradi uliosanifiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo ya Kigamboni, Kimbiji na maeneo ya jirani ambao walikuwa hawapati huduma.
HISTORIA FUPI YA MRADI
Wilaya ya Kigamboni ni eneo ambalo limekua na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji kwa muda mrefu kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa kupeleka huduma ya majisafi.
Changamoto hii ilisababisha wananchi wa Kigamboni kutumia gharama kubwa kununua maji kwa wauzaji binafsi ambayo nayo pia hayakua yakipatikana mara kwa mara.
Mwaka 2006 kulifanyika utafiti wa kutambua vyanzo vya maji vinavyoweza kutumika kutoa huduma ya maji kwenye Wilaya ya Kigamboni, ambapo waliangalia uwezekano wa kutoa maji baharini, kutoa maji kwenye mtambo wa Ruvu juu au chini, na tafiti nyingine iliangalia uwezekano wa kutumia maji yaliyopo chini ya ardhi (ground water).
Tafiti hiyo ijulikanayo kama Future Water City ilibainisha kuwa, matumizi ya maji yaliyopo chini ya ardhi ndio njia sahihi, nafuu na yenye ufanisi itakayoweza kufikisha maji kwa wakazi.
Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) iliipa kazi kampuni ya Serengeti kutafiti kwa kuchimba visima 3, vya majaribio vyenye kina cha mita 600 kwenda chini ili kubaini eneo lipi linatoa maji kwa wingi. Ambapo kupitia utafiti huo, walibaini eneo la Kimbiji ndilo lililoonekana kuwa na kiwango kikubwa cha maji chini ya ardhi.
Hivyo, kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa maji kwa wananchi wa Kigamboni, mwezi Machi mwaka 2013, DAWASA ilisaini mkataba na kampuni ya Serengeti Ltd wa kuchimba visima 20 vya kuzalisha maji kwa gharama ya Shilingi Bilioni 26 kwenye kata ya Kimbiji na Mpera.
Pia, DAWASA ilitilia saini na kampuni ya M/s Advent construction Ltd kwa ajili ya ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji la lita milioni 15 linalojengwa kwenye eneo la Kisarawe II, pamoja na kazi ya ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilomita 5.7 kutoka kituo cha kusukuma maji hadi kwenye tanki kubwa.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Mradi ulianza kutekelezwa na DAWASA kwa kutumia fedha za ndani shilingi bilioni 23 ambazo ni fedha za Serikali. Utekelezaji wa mradi wa maji Kigamboni umegawanyika katika sehemu kuu mbili.
Sehemu ya kwanza ya mradi (Lot 1);
Imehusisha ujenzi wa visima virefu saba vya kuzalisha maji vilivyojengwa Kimbiji na Kisarawe II, kisima 11, 13, 14, 15, 3, 5, na 9.
■ Kisima namba 11 kina urefu wa mita 415.8 na kina uwezo wa kuzalisha lita 450,000 za maji kwa saa.
■ Kisima namba 13 kina urefu wa mita 621.3 na kina uwezo wa kuzalisha lita 420,000 za maji kwa saa.
■ Kisima namba 14 kina urefu wa mita 603.5 na kina uwezo wa kuzalisha lita 300,000 za maji kwa saa.
■ Kisima namba 15 kina urefu wa mita 475.9 na kina uwezo wa kuzalisha lita 420,000 za maji kwa saa.
■ Kisima namba 3 kina urefu wa mita 447.2 na kina uwezo wa kuzalisha lita 100,000 za maji kwa saa.
■ Kisima namba 5 kina urefu wa mita 453.3 na kina uwezo wa kuzalisha lita 250,000 za maji kwa saa.
■ Kisima namba 9 kina urefu wa mita 449.9 na kina uwezo wa kuzalisha lita 450,000 za maji kwa saa.
Sehemu ya pili ya mradi (Lot II)
Imehusisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji la lita milioni 15, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kinachopokea maji kutoka kwenye visima na kupeleka kwenye tenki pamoja na ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kwa kutumia bomba za ukubwa wa inchi 28 kwa umbali wa kilomita 9.3.
Sambamba na hilo, mradi pia umehusisha ujenzi wa mtandao wa kusambaza maji kwenda kwa wananchi kwa umbali wa kilomita 65, kwa kutumia mabomba ya ukubwa wa 16 hadi inchi 3. Kazi ya ulazaji wa mabomba inatekelezwa kwenye maeneo ya Mjimwema, Kigamboni na Kibada imetekelezwa kwenye eneo la umbali wa kilomita 7.
Ujenzi wa Mtandao wa kusafirisha Maji Dar es Salaam
Kazi nyingine ambayo imefanyika kwenye mradi huu ni ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kutoka kwenye visima virefu vya Kibada kwenda Dar es Salaam kwenye umbali wa kilomita 9 kwa kutumia mabomba ya inchi 16.
Mkandarasi wa mradi huu ni kampuni ya ujenzi ya Advent ambayo imehusika na kazi ya ujenzi wa tenki kubwa la ujazo wa lita milioni 15, pamoja na uchimbaji wa visima 12 vya kuzalisha maji ilivyopo Kimbiji na Mpera, ambapo mpaka sasa visima 7 vimeshachimbwa na vimekamilika vyenye urefu wa mita 400 hadi 600 kila kimoja.
HALI YA UTEKELEZAJI WA MRADI KWA SASA
Mpaka sasa, utekelezaji wa mradi kwa awamu ya kwanza ya uchimbaji wa visima na kuzalisha maji imekamilika kwa asilimia 100 ambapo visima 7 vimeanza kutoa maji kikamilifu.
Pia utekelezaji wa mradi kwa awamu ya pili ikiwemo ujenzi wa tenki la lita milioni 15 pamoja na kituo cha kusukuma maji imekamilika kwa asilimia 100. Kazi inayoendelea ni ujenzi wa mtandao wa maji kwenda kwa wananchi kwa kutumia mabomba ya inchi 16 hadi 3 ambapo mpaka sasa wamelaza mabomba kwa umbali wa kilomita 20.
Pia ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kutoka kwenye visima virefu vya Kibada kwenda Dar es Salaam kwenye umbali wa kilomita 15 kwa kutumia mabomba ya inchi 16. umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wa katikati ya Jiji wameanza kupata huduma.
Baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa maji Kigamboni, Mamlaka inakusudia kutekeleza mradi pacha wa awamu ya pili Kigamboni ambao maandalizi yake yameanza katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23.
Mradi utahusisha kazi ya uendelezwaji wa visima vingine vinne vya kuzalisha maji vitakavyoongeza uzalishaji wa maji na kunufaisha wakazi wa Toangoma, Kongowe, Mbagala Zakiehm na Mbagala Kuu Wilayani Temeke.
WANUFAIKA WA MRADI
Mradi wa maji Kigamboni – Kimbiji umelenga kusambaza huduma ya maji kwa wakazi wapatao 250,000 pindi utakapokamilika mwezi Disemba mwaka 2022.
Maeneo yatakayonufaika na kukamilika kwa mradi huu ni pamoja na Wilaya yote ya Kigamboni na maeneo ya jirani