UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI MSHIKAMANO
UTANGULIZI
Uimarishwaji wa huduma ya majisafi kwenye maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ni mojawapo ya jitihada zinazotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuwezesha wananchi wa maeneo yote kupata huduma pasi na kikwazo chochote.
Mojawapo ya maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ni Kata ya Mbezi na Ubungo ambapo Serikali ya awamu ya Sita imewekeza fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka huduma kwenye eneo hilo.
Hivyo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ilisanifu mradi wa maji Mshikamano ili kuondoa shida ya maji kwenye Kata hizi na kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 95.
MADHUMUNI YA MRADI
Mradi huu ulisanifiwa na kutekelezwa kwa lengo la kukidhi agizo la Serikali la kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya mjini hususani Kata ya Ubungo, Kibamba na Mbezi.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Mradi ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 17.12.2021 kupitia mpango kazi ulioandaliwa kulingana na matakwa ya sheria.
Mradi umehusisha ulazaji wa bomba la ukubwa wa inchi 16 kwa umbali wa kilomita 0.35 kutoka kwenye bomba la inchi 30 linalosafirisha maji kutoka kwenye kituo cha kusukuma maji eneo la Mbezi Inn, ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha maji chenye tenki la kuhifadhi maji la ujazo wa lita 540,000 za maji, pamoja na ufungaji wa pampu.
Utekelezaji wa mradi umehusisha kazi mbalimbali ikiwemo;
Ulazaji wa bomba la ukubwa wa inchi 16 kwa umbali wa kilomita 0.35 kutoka kwenye bomba la inchi 30 linalosafirisha maji kutoka kwenye kituo cha kusukuma maji eneo la Mbezi Inn. Ujenzi wa bomba la kusafirisha maji la inchi 16 kwa umbali wa kilomita 2.7 kutoka kwenye kituo cha kusukuma maji Mbezi Inn, hadi kwenye tanki kuu la kuhifadhi na kusambaza maji.
Ujenzi wa tenki kubwa la lita milioni 6 lililopo eneo la Mshikamano juu. Ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha maji chenye uwezo wa kuhifadhi lita 540,000 za maji, kazi ambayo imefanyika sambamba na kufunga pampu kwenye kituo hicho.
Mradi una uwezo wa kusafirisha lita milioni 23,300 za maji kwa siku ambazo zinatosheleza mahitaji ya wananchi 179,476 kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
MAENEO YANAYONUFAIKA NA MRADI
Mradi unategemewa kunufaisha wakazi wa Kata ya Mshikamano, Mpiji – Majohe, Msakuzi Kusini, Msakuzi A, Machimbo, Majengo mapya, Dodoma pamoja na vitongoji vyake.
GHARAMA ZA MRADI
Mradi umetekelezwa kwa gharama ya bilioni 4.8. Kati ya fedha hizi, bilioni 2.5 ni fedha kutoka Serikali kuu kutoka mfuko wa UVIKO 19, na bilioni 2.3 ni fedha za ndani kutoka DAWASA. Mradi umetekelezwa na Mkandarasi M/S Advent Co. Ltd chini ya usimamizi wa DAWASA.
HATUA YA UTEKELEZAJI WA MRADI
Utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na kazi inaendelea ya kuunganisha wateja na huduma ya majisafi