MRADI WA MAJI MLANDIZI – CHALINZE – MBOGA
UTANGULIZI
Mradi wa maji Mlandizi – Chalinze - Mboga ni mojawapo ya mradi wa kimkakati uliosanifiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kukamilika Julai mwaka 2021. Mradi ulitekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya Advent chini ya usimamizi wa Serikali ya awamu ya Sita.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Mradi huu umetekelezwa chini ya DAWASA na umekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Chalinze waliokuwa na shida kubwa ya ukosefu wa maji.
Mradi huu una uwezo wa kusafirisha kiasi cha lita milioni tisa na laki tatu (9,300,000) za maji kwa siku na kunufaisha wakazi wapatao 120,912 kwa siku.
KAZI ZILIZOTEKELEZWA KWENYE MRADI
Ulazaji wa bomba kubwa la inchi 16 kwa umbali wa kilomita 59 kutoka kwenye Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu mpaka Chalinze, na kufika kijiji cha Mboga, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji kijiji cha Chamakweza na Msoga.
Ujenzi wa maunganisho maalum katika maeneo ya Mlandizi, Ruvu (Nelo), Vigwaza mizani, Chamakweza, Pingo, Pera, Chalinze, Msoga, Mboga sayona na Mboga matenki ya maji.
MAENEO YATAKAYONUFAIKA NA MRADI
Maeneo ambayo yamenufaika na mradi huu ni pamoja na maeneo ya viwanda vya Twyford, KEDA, Kiwanda cha ngozi, bandari kavu ya Vigwaza, Kiwanda cha sayona, stesheni ya treni ya mwendokasi, Vigwaza (kwala), Kituo cha mizani – Vigwaza.
Maeneo mengine ni pamoja na Kijiji cha Mboga, Chamakweza, Chahua, Lukenge, Nhelo, Ruvu darajani, Kidogozero, Mdaula – Ubena zomozi, Bwawani, Buyuni, Visezi, Vigwaza, Pingo, Pera, Bwiligu, Chalinze mjini, Chalinze mzee na Msoga.
Kupitia utekelezaji wa mradi huu, Mamlaka imefanikiwa kusanifu mradi mwingine wa kupeleka maji eneo la Kwala, Chalinze na eneo la Ruvu darajani.
Utekelezaji wa mradi umegharimu kiasi cha bilioni 18 ambazo ni mapato ya ndani ya Mamlaka na kazi imekamilika kwa asilimia 100 na wakazi tajwa wa Chalinze wameanza kupata maji.
Kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa haraka wa maji kwa wananchi, Serikali kupitia agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa shilingi milioni 500 kwa lengo la kuwezesha zoezi la maunganisho ya haraka ya maji kwa wakazi wa Chalinze.