MRADI WA MAJI MKURANGA
Mradi wa maji Mkuranga ni mojawapo ya mradi wa kimkakati uliosanifiwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani.
HISTORIA YA MRADI
Wilaya ya Mkuranga iliyoko Mkoa wa Pwani ni mojawapo ya eneo lililokuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na kutokuwa na miundombinu ya majisafi ya DAWASA.
Mkuranga huwa inapata misimu miwili ya mvua yaani masika na vuli. Wastani wa mvua hizi ni milimita 800 hadi 1,000 kwa mwaka. Mvua za masika kawaida hunyesha kati ya miezi ya Machi hadi Juni, na mvua za vuli hunyesha kati ya miezi ya Oktoba hadi Disemba.
Katika miaka ya hivi karibuni mvua hizo zimekuwa ni haba kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Hali hii imechangia sana kukauka kwa vyanzo vya maji, hususani katika maeneo yenye huduma ya maji ya visima vifupi.
Vyanzo vikuu vya maji katika Wilaya ya Mkuranga vimekuwa ni uvunaji wa maji ya mvua, maji ya chini ya ardhi (Underground Water), chemichemi na mabwawa. Mpaka Juni, 2017 jumla ya wakazi 123,623 wamekuwa wakipata huduma ya majisafi kupitia vyanzo hivyo.
Hii ni sawa na asilimia 62.5 ya wakazi wote 197,797 wa Mkuranga waishio vijijini. Vilevile asilimia kumi (10) ya wakazi wa mji wa Mkuranga ndio wanaopata huduma ya majisafi.
UPATIKANAJI WA HUDUMA YA MAJI
Mpaka kufikia tarehe 30 Juni 2017, huduma ya maji katika Wilaya ya Mkuranga maeneo ya vijijini imekuwa ikipatikana kwa wastani wa asilimia 62.5. Aidha, huduma hii hutolewa kwa kutumia miundombinu ya maji ya mitandao ya bomba, visima virefu na vifupi vya pampu za mkono, zinazoendeshwa na mitambo ya genereta za nishati ya mafuta, umeme wa nguvu ya jua na mifumo ya kuvuna maji ya mvua.
Aidha, jumla ya wakazi 2,512 wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Mkuranga, wamekuwa wakipata majisafi sawa na asilimia 10 ya wakazi wote wa mji. Mji huu hupata maji kutoka katika chanzo cha kisima kirefu kilichopo eneo la Kulungu.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi umehusisha kazi mbalimbali zikiwemo;
Ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji la lita milioni 1.5 Ujenzi wa chanzo cha kuzalisha maji chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 6.8 ambayo ni sawa na lita 284,000 kwa saa moja.
Ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji kwa umbali wa kilomita 63 katika mji mzima wa Mkuranga. Pia ujenzi wa mtandao wa bomba kubwa la kutoa maji kwenye kisima kwenda kwenye tanki kwa umbali wa kilomita 1.3.
Ujenzi wa kituo cha kusukuma maji chenye uwezo wa kusukuma lita 540,000 za maji. Utekelezaji wa mradi huu umeweza kunufaisha wakazi 25,000 wa Wilaya ya Mkuranga ambao walikuwa hawapati huduma ya majisafi hapo awali.
Mradi umetekelezwa na DAWASA na umegharimu shillingi bilioni 5.5, na sasa mradi umekamilika kwa asilimia 100. Mradi huu ulizinduliwa na Kiongozi wa mbio za mwenge Sahil Geraruma Mei, 2022.
Katika awamu ya pili, mradi unalenga kuunganisha ukanda mzima wa Wilaya ya Mkuranga mpaka maeneo ya Kongowe hadi Mbagala.
Awamu ya pili ya mradi itahusisha ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji lenye uwezo wa kubeba lita milioni sita litakalojengwa maeneo ya Mwanambaya ili kutatua changamoto ya maji kwenye Wilaya yote ya Mkuranga na vijiji vyake.
Mradi umetekelezwa na kukamilika kwa asilimia 100 na mradi unaendelea kutoa huduma kwa wateja wote walengwa wa Mkuranga. Mpaka sasa mradi umeweza kuwaunganisha wateja mbalimbali wapatao 2457 wa Kata ya Mgawa, kitumbo, ngunguti, terminal, kiguza, mkwalia, buganyama, miale, kikungo, mikwambe, mwinyi, ujenzi na panone.