MRADI WA KUSAMBAZA MAJI KUTOKA MAKONGO HADI BAGAMOYO
UTANGULIZI
Mradi wa kusambaza maji Makongo hadi Bagamoyo ni mojawapo ya mradi wa kimkakati unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Makongo Jijini Dar es Salaam hadi Wilaya ya Bagamoyo.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Mradi huu unatekelezwa kupitia wafadhili wa maendeleo chini ya usimamizi wa DAWASA kupitia mkandarasi wa kampuni ya CDEIC & HAINAN Joint Ventur, aliyehusika na ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhi maji ya ujazo wa lita milioni 5, yaliyojengwa maeneo ya Vikawe, Mbweni na Tegeta A, pamoja na ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji vinavyojengwa eneo la Vikawe na Mbweni.
Mradi huu umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa gharama ya bilioni 65.4 ikiwa ni ushirikiano na Benki ya Dunia (WB).
KAZI ZILIZOTEKELEZWA KWENYE MRADI
Utekelezaji wa mradi umehusisha kazi mbalimbali zikiwemo;
Ujenzi wa matenki matatu ya kuhifadhi maji yaliyojengwa kwenye maeneo ya Vikawe, Mbweni na Tegeta A yenye ujazo wa lita milioni 5 kila moja. Pia ujenzi wa vituo vya kusukuma maji vinavyojengwa eneo la Vikawe na Mbweni, ulazaji wa mabomba makubwa ya maji ya inchi 16, 12, 10 kwa umbali wa kilomita 1,219 pamoja na mabomba ya kusambaza maji kwa umbali wa kilomita 1,442.
Ujenzi wa mtandao wa mabomba madogo na makubwa ya kusafirisha na kusambaza maji ya kuanzia inchi 2.5 hadi inchi 16 kwa umbali wa 1,252. Mpaka sasa, ujenzi wa tenki la Tegeta A na Vikawe umekamilika kwa asilimia 98.6, na tenki la Mbweni limekamilika kwa asilimia 100.
Kazi nyingine ni pamoja na maunganisho ya maji kwa wateja ambapo wateja wapya 7,740 wa Bunju wameunganishwa, Bagamoyo wateja 1,910, Mbweni wateja 145 na Wazo wateja 565 wameunganishwa.
HALI YA UTEKELEZAJI WA MRADI KWA SASA
Utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na kazi ya kuunganisha wateja kwenye maeneo yote yaliyoainishwa inaendelea.
MAENEO YANAYONUFAIKA NA MRADI
Mradi huu umelenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa zaidi ya wateja 450,000 wa maeneo yafuatayo;
Kwa Wilaya ya Kinondoni mradi unahudumia wakazi wa Changanyikeni, Vikawe, Goba, Mivumoni, Mbweni, Madale, Tegeta A, Bunju, Wazo, Ocean-bay na Salasala. Kwa upande wa Bagamoyo mradi utahudumia wakazi wa Kata za Mataya, Sanzale, Migude, Ukuni, Mtambani, Nianjema, Kimara ngo’mbe, Kisutu, Block P.
Kwa eneo la Vikawe, mradi utahudumia Kata ya Mapinga, kwa matumbi na Vikawe bondeni. Kwa upande wa Mabwepande, mradi utahudumia kata ya Bunju B, Mabwepande na Mbopo, na Kata ya Salasala mradi utahudumia Salasala, Kinzudi, Mbezi, Goba na Kilongawima.