MRADI WA MAJI KITOPENI
Mojawapo ya adhma ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wa maeneo yote wanapata huduma bora ya majisafi ya uhakika na kwa muda wote pasi na shida yoyote.
Katika kufanikisha hili, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imetekeleza mradi wa kusambaza maji kwa wakazi wa maeneo ya Mbezi Makabe na Msakuzi Kusini, Wilaya ya Ubungo.
UTANGULIZI;
Mradi wa maji Kitopeni ni mojawapo ya mradi uliosanifiwa na kutekelezwa na DAWASA kwa lengo la kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji kwa wakazi wa maeneo ya Mbezi Makabe na Msakuzi Kusini.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Mradi umetekelezwa na Mkandarasi wa kampuni ya SAMKA, kwa kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Mei mwaka 2022 na kukamilika mwezi Novemba mwaka 2022. Mradi umetekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya DAWASA kiasi cha shilingi milioni 740,651,675.
Mradi umechukua maji kutoka kwenye chanzo cha maji ya bomba kubwa la inchi 36 na kwenda kwenye bomba la inchi 6 linalopeleka maji kwenye tenki.
Kazi nyingine zilizotekelezwa kwenye mradi ni pamoja na;
Ujenzi na ulazaji wa mtandao wa mabomba ya inchi 6 kwa umbali wa kilomita 3.32. Ufungaji wa pampu 2 za kusukuma maji zenye uwezo wa kusukuma lita 120,000. Kufunga mabomba ya kupandisha na kushusha maji kwenye tenki la lita elf 90 lililorithiwa kutoka Manispaa ya Ubungo.
Mradi umenufaisha wananchi zaidi ya wakazi 30,000 wa Kata ya Mbezi Makabe, Wilaya ya Ubungo. Kwa sasa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na kazi ya kuunganisha wananchi na huduma ya majisafi inaendelea kwenye maeneo mbalimbali.