Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
TAARIFA YA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI CHALINZE AWAMU YA TATU
TAARIFA YA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI CHALINZE AWAMU YA TATU

Mradi wa Maji Chalinze awamu ya tatu ni mojawapo ya miradi ya kimkakati uliosanifiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Pwani, Ngerengere na baadhi ya vijiji vya Mkoa wa Morogoro.

Mradi ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 na DAWASA kupitia Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya ujenzi ya Afcons (Afcons Construction Limited) kwa lengo mahususi la kuondoa tatizo la upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Halmashauri ya mji wa Chalinze.

Kutokana na changamoto ya maji iliyokwepo kwenye eneo hili, Serikali ya awamu ya sita iliwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi, ambapo kutokana na makubaliano na Benki ya Exim ya India, serikali iliwezesha kupatikana kwa dola milioni 48 za kutekeleza mradi huu.

Utekelezaji wa mradi huu ulihusisha kazi mbalimbali zikiwemo;

Kazi ya upanuzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Wami kwa lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji maji kutoka lita milioni 7.2 za sasa mpaka lita milioni 9, ili kuongeza uzalishaji wa maji na kuweza kuhudumia wakazi wa Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, baadhi ya vijiji vya mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani na eneo la Ngerengere.

Kazi ya ujenzi wa matenki 19 ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 500,000 mpaka lita milioni 2 ambayo yamejengwa kwenye maeneo ya Kimange, Rupungwi, Mandela, Hondogo, Kilemela, Miono, Msata, Kihangaiko, Mazizi, Saleni, Lugoba, Mindutulieni, Diozile, Msoga, Bwiligu, Mpera, Pingo, Manga na tenki la Majisafi Mtamboni.

Pia mradi umehusisha kazi ya ujenzi wa vioski (vizimba) 351 vya kuchotea maji vinavyojengwa kwenye vijiji zaidi ya 69, baadhi ya hivyo ni; kijiji cha Msingi, Mdaula, Msolwa, Visakazi, Kikaro, Buyuni, Mandamazingara na kijiji cha Mboga kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa urahisi kwa vijiji zaidi ya 69.

Mbali na hapo, mradi umejenga mtandao wa mabomba makubwa ya inchi 12 na 16 ya kusafirisha maji kwa umbali wa kilomita 24, pamoja na ujenzi wa mabomba ya kusambaza maji kwa umbali wa kilomita 1,268.

 

 

 

 

WANUFAIKA WA MRADI

Utekelezaji wa mradi huu mkubwa umelenga kutoa huduma kwa zaidi ya wakazi 200,000 wa Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Pwani, baadhi ya vijiji vya Mkoa wa Morogoro na eneo la Ngerengere.

Mradi unatarajiwa kunufaisha wakazi wa Halmashauri ya Chalinze, sehemu ya Kata zilizopo Tanga, Mkata, Morogoro na Bwawani Mkoa wa Pwani. Pia Kata ya Kiwangwa, Msata, Miono, Magomeni, Vigwaza, Tarawanda, Bwirigu, Ubena zomozi, Mbwewe, Lugoba, Fukayose, Mpera, Msoga kimange, Mandela, Gwata, Magigu, Mkata kwa sungu, Ngerengere na Kidugalo.

Kupitia utekelezaji huu, mradi utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 22 za maji kwa siku ambayo ni ziada ya mahitaji ya maji kwa Halmashauri ya Chalinze ya lita milioni 7 – 9 kwa siku.

 

HALI YA UTEKELEZAJI WA MRADI KWA SASA

Mpaka sasa utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na kazi inayoendelea ni kuunganisha wateja kwenye mfumo wa usambazaji maji.