Miradi
UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI MLANDIZI – CHALINZE – MBOGA
UTANGULIZI
Huu ni mojawapo ya miradi ya kimkakati….
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetekeleza mradi wa maji Mlandizi - Chalinze - Mboga unaolenga kuondoa shida ya upatikanaji wa majisafi kwa mji mzima wa Chalinze.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya kimkakati uliosanifiwa kwa lengo la kusafirisha kiasi cha lita milioni tisa na laki tatu 9,300,000 kwa siku na kunufaisha wakazi wapatao 120,912 kwa siku.
UTEKELEZAJI WA MRADI
Utekelezaji wa mradi umehusisha ulazaji wa bomba kubwa la inchi 16 kwa umbali wa kilomita 59 kutoka kwenye Mtambo wca kuzalisha maji wa Ruvu Juu mpaka Chalinze na kufika kijiji cha Mboga, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji kijiji cha Chamakweza na Msoga pamoja na ujenzi wa maunganisho maalum katika maeneo ya Mlandizi, Ruvu (Nelo), Vigwaza mizani, Chamakweza, Pingo, Pera, Chalinze, Msoga, Mboga sayona na Mboga matenki ya maji.
MAENEO YANAYONUFAIKA NA MRADI
Maeneo yatakayonufaika na mradi ni pamoja na maeneo ya viwanda vya Twyford, KEDA, kiwanda cha ngozi, bandari kavu ya Vigwaza, kiwanda cha sayona, stesheni ya treni ya mwendokasi, Vigwaza (kwala) na kituo cha mizani – Vigwaza.
Maeneo mengine ni pamoja na kijiji cha Mboga, Chamakweza, Chahua, Lukenge, Nhelo, Ruvu darajani, Kidogozero, Mdaula – Ubenazomozi, Bwawani, Buyuni, Visezi, Vigwaza, Pingo, Pera, Bwiligu, Chalinze mjini, Chalinze mzee na Msoga.
Utekelezaji wa mradi umegharimu kiasi cha bilioni 18 ambazo ni mapato ya ndani ya Mamlaka.
Utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia asilimia 100, kazi zote zilizotarajiwa kutekelezwa zimekamilika.