WATUMISHI WAKUMBUSHWA MIONGOZO YA UTUMISHI WA UMMA
Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wamekumbushwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa lengo kuongeza na kuboresha ufanisi wa kazi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) Ndugu Neema Wilbard wakati wa mafunzo maalum ya kuhusu miongozo ya utendaji kazi mahali pa kazi ili kuongeza uzalishaji na kuboresha utoaji wa huduma za majk kwa wateja wote wanaohudumiwa.
Amesema kuwa ni muhimu kwa watumishi wa Umma kupewa elimu hii ya kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kujua majukumu yao, mipaka yao pamoja na wajibu wao katika utekelezaji wa kazi za kila siku.
"Sheria imeainisha makosa na adhabu mbalimbali ambazo mtumishi wa umma anatakiwa azifahamu ili kuepuka adhabu zinazoweza kumpata, hivyo ni vyema kila Mtumishi afahamu haya," ameeleza Bi Neema.
Ameongeza kuwa elimu hii imelenga kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa Mamlaka kwa kujiepusha na vitendo vilivyo nje ya utaratibu wa Sheria.
"Tunawasihi watumishi wa Mamlaka kuzingatia taratibu hizi na Sheria zilizopo ili kuongeza tija kwa wateja wanaohudumiwa kwenye maeneo yote ya Dar es Salaam na Pwani," ameeleza Bi Neema.
Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo mmoja wa washiriki wa mafunzo Bi Magreth Yameti amesema kuwa elimu kutoka TUICO imekuwa ya msaada sana kwa kuwa itasaidia kujua sheria mbalimbali za utumishi wa umma, makosa na adhabu zake ili kuwa na uelewa mpana wa namna ya kuongeza ufanisi na kujiepusha na makosa yanayoweza kuhatarisha ajira na kuharibu utendaji wa kazi.
Amesema pia kuwa kupitia mafunzo haya, yataenda kuboresha utoaji wa huduma kwa weledi kwa wananchi wote.