WATUMISHI DAWASA WAPEWA ELIMU YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wamepatiwa elimu juu ya mfumo mpya wa kieletroniki wa kupata taarifa mbalimbali za mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSF portal.
Afisa Matekelezo kanda ya Kinondoni PSSSF, Ndugu Herrieth Shoo amesema ni muhimu kwa watumishi wa DAWASA kufahamu manufaa na huduma zitolewazo na mfuko wa PSSSF kipindi wawapo kazini na hata kipindi watakapostaafu.
"Serikali imehakikisha wafanyakazi katika sekta ya umma wananufaika na mifuko ya mafao, tunaamini kwa elimu hii, watumishi wa DAWASA sasa watakuwa na uwezo wa kutumia mfumo wetu wa kidijitali ambao utasaidia uhifadhi sahihi wa taarifa za wanachama pamoja na ufuatiliaji michango na huduma nyingine," amesema Ndugu Herieth.
Ndugu Herrieth ametoa rai kwa watumishi wa DAWASA kuwa mabalozi wazuri kwa kutoa elimu juu ya mfumo huu pamoja na manufaa yake kwa watumishi wengine ili kujenga zao la watumishi bora.
Afisa Rasilimali watu DAWASA, Ndugu Neema Kamaghe amesema uwepo wa mafunzo hayo ni muendelezo wa jitihada za DAWASA kuhakikisha watumishi wanapata uelewa wa mambo mbalimbali katika eneo la kazi hususani usalama wa mafao yao.
"Mafunzo haya ni miongoni mwa mikakati ya DAWASA katika kuhakikisha kila mtumishi anakuwa na uelewa na shughuli mbalimbali zinazogusa kazi zake na muktabari wa maisha yao wawapo kazini na baada ya kustaafu, na kupitia mafunzo haya kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa taarifa pamoja na kuongeza uelewa kwa watumishi kuhusu masuala mbalimbali ya mfuko wa hifadhi za jamii," ameeleza.