Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI TALIANI - KISARAWE WAHAKIKISHIWA UPATIKANAJI WA HUDUMA
29 Sep, 2023
WAKAZI TALIANI - KISARAWE WAHAKIKISHIWA UPATIKANAJI WA HUDUMA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na kuongea na Wakazi wa Mtaa wa Taliani kuhusu upatikanaji wa majisafi na kueleza mikakati iliyopo ya kuimarisha huduma ikiwemo utekelezaji wa mradi wa kuongeza msukumo wa maji Taliani, kufungwa kwa pampu mpya ya Kibamba pamoja na ukamilishwaji wa mradi wa maji Yangeyange.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Kisarawe Ndugu Alex Ng'wandu wakati wa kikao na wananchi wa mtaa huo kuelezea jitihada zinazofanywa na Mamlaka za kusogeza huduma kwenye maeneo yao.

Amesema kuwa Mamlaka inaelewa adha ya ukosefu wa maji wanayoipata wananchi wa maeneo haya ikiwemo baadhi ya maeneo kupata maji kwa msukumo mdogo na maeneo mengine kutokuwa na huduma kabisa.

Ameongeza kuwa mipango iliyopo ya kuboresha huduma inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na mradi wa TFS Taliani wa kuongeza msukumo wa maji, kufungwa kwa pampu mpya ya Kibamba itakayosaidia kuongeza msukumo wa maji kwa wingi kwenda kwenye tenki la maji. Kazi nyingine ni kukamilisha utekelezaji mradi wa maji Yangeyange unaolenga kunufaisha wakazi wa mtaa wa Yangeyange, Kata ya Msongola. 

"Naomba niwaeleze tu kwamba, changamoto ya ukosefu wa maji katika eneo hili inajulikana na Mamlaka inafanya kila jitihada kuhakikisha maji yanapatikana kwa kuwa ni haki ya kila mwananchi kupata maji, hivyo muwe na uvumilivu," ameeleza Ndugu Ng'wandu.

Mbali na hapo, Meneja alitumia wasaa huo kupokea na kujibu malalamiko mbalimbali ya wananchi yanayohusu upatikanaji wa huduma.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Kisarawe Ndugu Eliamini Mshana ameipongeza Mamlaka kwa kuona adha iliyopo kwenye eneo hili na kuchukua hatua madhubuti ya kutatua.

"Hii kwetu ni faraja maana eneo hili limekuwa na changamoto ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu, mpaka wananchi wanaenda kutafuta maji mbali na makazi yao," ameeleza Ndugu Mshana na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati kazi ikiendelea kutekelezwa ya kufikisha maji kwenye eneo hili.

Mkazi wa mtaa wa Tuliani, Ndugu Erica Mwamboke ameeleza tabu wanayoipata ya kukosa maji kwa muda mrefu ambapo wanalazimika kutumia gharama kubwa kununua maji kutoka mbali.

Ameiomba DAWASA kuongeza nguvu katika miradi hii ili waweze kupata maji na kuondokana na adha ya muda mrefu.