Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
USAMBAZAJI MAJI KIBADA, VIJIBWENI, MJIMWEMA NA TUNGI WASHIKA KASI 
06 Sep, 2023
USAMBAZAJI MAJI KIBADA, VIJIBWENI, MJIMWEMA NA TUNGI WASHIKA KASI 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na kazi ya usambazaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi wa Kigamboni kupitia utekelezwaji wa mradi mkubwa wa maji wa Kigamboni. 

Kazi ya usambazaji maji kwa wananchi imeendelea kwa kasi ambapo mpaka sasa zoezi la ulazaji wa mabomba makubwa na madogo limetekelezwa kwa takribani asilimia 70. 

Akielezea utekelezaji wa mradi huu wa usambazaji maji, Msimamizi wa mradi Mhandisi Farida Kyamani wa DAWASA amesema kuwa mpaka sasa jumla ya kilomita 120 za mabomba ya maji yamelazwa. 

Amefafanua kuwa, maeneo yaliyolazwa bomba ni pamoja na Kibada hadi kwa Mwingira, mradi umelaza bomba la inchi 16, Kibada hadi vijibweni wamelaza bomba la inchi 12, pamoja na kutoka Ungindoni mpaka Kibugumo ambapo wamelaza bomba la inchi 12. 

Amebainisha kuwa Kata ambazo tayari mabomba ya maji yamefika ni pamoja na Kata ya Kibada, Kisarawe II, Somangila, Vijibweni, Mjimwema, feri, tungi na Kigamboni. Ambapo kwa mitaa ni pamoja na Uvumba, Kifurukwe, Feri, Tungi, Magogoni, Ungindoni, Kiziza na Kisota. 

“Baada ya kazi ya ulazaji wa mabomba makubwa ya inchi 16 na 12, kazi kubwa imefanyika ya kutoa matoleo ya inchi 8, 6, 4 na 3 na kusambaza maji kwa wananchi wa mitaa iliyoainishwa ili wapate huduma ya maji,” ameeleza Mhandisi Farida. 

"Eneo linalobaki la kusogeza huduma karibu na wananchi ni kazi inayofanywa na Mkoa wa kihuduma DAWASA Kigamboni," ameeleza Mhandisi Farida. 

Ameeleza kuwa kazi inaendelea ya kulaza mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi kwa mitaa iliyobaki ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji kwa wananchi wote. 

Mradi wa maji Kigamboni umetekelezwa kwa gharama ya bilioni 23 ikiwa ni fedha kutoka Serikalini na kuhusisha ujenzi wa tenki la ukubwa wa lita milioni 15. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kata ya Kibada Abraham Mguna amesema kuwa kazi inayoendelea kwenye kata na mitaa mbalimbali inawapa moyo wananchi kupata maji. 

"Niwapongeze DAWASA kwa jitihada zinazoendelea za kuboresha huduma ya maji, tunaomba Mamlaka iongeze nguvu za kutekeleza mradi huu ili wananchi wapate maji," amesema. 

Akielezea matumaini ya upatikanaji wa maji kwenye eneo lao, Ndugu Erica Danstan mkazi wa Tungi ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa jitihada kubwa za kufikisha maji kwenye eneo lao, maana wamekuwa kwenye shida ya maji kwa muda mrefu. 

Ameeleza kuwa kwa sasa wanamatumaini ya kupata maji maana wameona kazi inayoendelea kutekelezwa kwenye mitaa yao. 

"Ninaimani kubwa kwa Mamlaka kwamba maji yatafika, tayari nimeona mabomba yakilazwa na kazi ya maunganisho mapya inaendelea," ameeleza Ndugu Erica.