Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
UJENZI WA VITUO VYA HUDUMA KWA UMMA DAR WAFIKIA ASILIMIA  90
15 Sep, 2023
UJENZI WA VITUO VYA HUDUMA KWA UMMA DAR WAFIKIA ASILIMIA  90

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi wa ujenzi wa vituo vya kutolea huduma kwa umma takribani 30 vinavyojengwa kwenye Wilaya 5 katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo Kinondoni, Temeke, Kigamboni, Ilala na Ubungo, kwa lengo la kuboresha usafi wa mazingira katika maeneo ya umma.

Mradi huu ambao kwa sasa umefikia asilimia 90, unatekelezwa na DAWASA kwa ushirikiano wa Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi billioni 3.2.

Akizungumzia maendeleo ya utekelezaji wa mradi huu, Msimamizi wa mradi Mhandisi Hamad Msemo amesema kuwa miradi hii imejengwa katika maeneo yenye muingiliano mkubwa wa wananchi kama vile sehemu za masoko na stendi za mabasi.

"Leo hii tuko katika moja ya maeneo ambayo mradi huu unatekelezwa eneo la Shekilango Wilaya ya Ubungo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Shekilango ambapo upo katika hatua za mwisho za  ukamilishwaji " ameeleza Mhandisi Msemo.

Katibu wa Soko la Shekilango, Charles Shirima amesema kuwa mradi huu unaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo haya hususani wafanyabiashara wa soko hili, kwa kuwa huduma ya choo ni ya umuhimu kwa kila mtu.

"Ni shauku ya kila mwananchi kuhudumiwa na vituo hivi kwa kuwa vimejengwa kwa ubora na kwa kuzingatia viwango vya hali ya juu," amesema.

Mfanyabiashara wa soko hilo, Vanessa Silayo ameipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa jitihada za kujenga vituo hivi vinavyosaidia kuboresha afya zetu na kutuondolea hatari ya magonjwa ya mlipuko.

"Mradi huu umetuletea nafuu kubwa kwa kuwa umejengwa vizuri na kisasa, hivyo hatuna wasiwasi wa uwepo wa magonjwa ya mlipuko," ameeleza Ndugu Vanessa.