Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
UJENZI WA BWAWA LA KIDUNDA WASHIKA KASI MOROGORO
09 Feb, 2024
UJENZI WA BWAWA LA KIDUNDA WASHIKA KASI MOROGORO

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Maji kidunda Mkoani Morogoro, unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es salaam na Pwani umeshika kasi huku utekelezaji wake ukifikia asilimia 15.

Akiongea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, msimamizi wa mradi huo kutoka DAWASA, Mhandisi Christian Christopher ameeleza kuwa utekelezaji wa kazi mbalimbali unaendelea kama ilivyo katika mkataba wa mkandarasi.

"Kazi zinazoendelea kwasasa ni pamoja na kusafisha barabara inayotoka Ngerengere hadi kijiji cha Kidunda zaidi ya kilomita 17 kwajili ya ujenzi, ujenzi wa kingo za mto, uchombaji wa eneo la bwawa, utayarishaji na upasuaji wa mawe kwa ajili ya ujenzi, pamoja na kutengeneza tofali zinazotumika katika kujenga nyumba za watumishi." ameeleza Mhandisi Christopher.

Mhandisi Christopher ameongeza kuwa ujenzi wa njia ya umeme toka Kidunda kwenda kituo cha kupooza umeme Chalinze ipo katika hatua za usanifu na ujenzi utaanza mara baada ya kukamilika kwa hatua hiyo.

Katika hatua nyingine Mhandisi Christopher amebainisha kazi zilizokamilika tangu kuanza kwa mradi hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za muda za mkandarasi, kufunga mtambo wa kusaga mawe, pamoja na kufanga mtambo wa kutengeneza zege.

Sambamba na kuhifadhi maji mengi yatakayotumika katika kipindi cha upungufu wa mvua, ujenzi wa mradi wa bwawa la kidunda unatajwa kuwa na faida nyingi ikiwemo uzalishaji wa umeme megawati 20, kutengeneza ajira takribani 1,000, uboreshwaji wa miundombinu ya barabara kutoka katika vijiji nufaika na mradi kama vile Ngerengere hadi kijiji cha Kidunda pamoja na kuchangia ukuaji wa shughuli za uvuvi pamoja na kuwa sehemu ya kivutio cha utalii.

Ujenzi wa bwawa la kidunda utakaogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Bilion 300, utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia Juni 2023 hadi Juni 2026.